Walimu 437 Kahama kupelekwa kutalii mbugani kuondoa ‘stresi’

Kahama. Zaidi ya walimu 437 wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wanatarajiwa kupelekwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kutalii, ili kupunguza msongo wa mawazo unaosababisha changamoto ya matatizo ya afya ya akili.

Hatua hiyo inakuja ili kuwaweka sawa walimu kiakili na kuwapunguzia msongo wa mawazo  unaosababisha  kuwafanyia ukatili wanafunzi.

Hiyo ni baada ya hivi karibuni kutokea tukio la mwanafunzi kufariki dunia baada ya kuchapwa na mwalimu wake mkoani Simiyu.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, ametoa ahadi hiyo leo Machi 26,2025 wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kahama, na kusema amefikia hatua hiyo  kama njia mojawapo ya kupambana na changamoto ya afya ya akili kwao, na kuimarisha utendaji kazi wa walimu wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Mboni Mhita akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama cha walimu Tanzania (CWT) leo Machi 26, 2025. Picha na Amina Mbwambo

Amesema baadhi ya walimu wamekuwa waathirika wa vitendo vya ukatili kwa wanafunzi wao, huku wengi wao wakionekana kuwa na msongo wa mawazo unaosababisha changamoto ya afya ya akili, ambayo wakati mwingine si vyepesi kugundulika kwa kuangalia kwa macho.

“Kazi na dawa na ili mtu asiwe na msongo wa mawazo, aendelee kuimarisha afya ya akili, lazima mambo kama haya yafanyike, mtaenda mbuga za wanyama mkabadilishe mazingira, mkirudi darasani muwe wapya muendelee na kazi, lakini pia tuendelee kuzuia vitendo vya ukatili kwa wanafunzi wetu tunavyovishuhudia katika maeneo mengine.”

“Unakuta mwalimu anachapa tu mtoto kwa kusema si mwelewa, kumbe mtoto anaelewa, nimeona twendeni mbugani na mimi nitalisimamia hili,” amesema.

Mwalimu Revocatus Patrick kutoka Shule ya Msingi Busangi Halmashauri ya Msalala, amesema hatua hiyo itamsaidia mwalimu kufundisha mambo anayoyafahamu, tofauti na sasa mwalimu anamfundisha mwanafunzi kuhusu tembo, lakini hata hajawahi kumuona.

Amesema “Kuna wengine tunafundisha watoto mbuga za wanyama zilizopo Tanzania, lakini hatujawahi kufika, unamfundisha tembo ila hata mwalimu tu hajawahi kumuona, hii inakuwa haina msisitizo sana, lakini wazo la kwenda huko ni zuri sana kwetu.”

Naye mwalimu Stella Silayo wa Shule ya Msingi Mtakuja Manispaa ya Kahama amesema safari hiyo itamsaidia kubadilisha mazingira na kupunguza msongo wa mawazo na atakavyotoka sivyo atakavyorudi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *