
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema watatoa maelezo yao mbele Mahakama baada ya yeye na viongozi wenzake kushikiliwa na kuachia kwa dhamana na Jeshi la Polisi.
Mbowe aliyekuwa Kituo cha Osterbay, amesema hayo jana Jumatatu usiku Septemba 23, 2024 alipozungumza na waandishi na wafuasi wa Chadema baada ya kuachiwa.
Amesema hakuna kilichoendelea wakiwa mikononi mwa polisi, yeye na wenzake wameachiwa kwa dhamana bila masharti yoyote.
“Bado sijapata taarifa rasmi ya viongozi wenzangu wana hali gani kwa sababu tulikamatwa maeneo tofauti, tumewaambia polisi hatutatoa maaelezo yoyote hadi tutakapopelekwa mahakamani, mbele ya mahakimu na majaji,” amesema Mbowe.
Mbowe, wanachama na viongozi wengine walikamatwa kwa nyakati tofauti jana Jumatatu, Septemba 23, 2024 jijini Dar es Salaam wakijiandaa na maandamano waliyoyaita ya maombolezo na amani.
Maandamano hayo yalikuwa na lengo la kupinga matukio ya utekaji na mauaji ya wanachama wa chama hicho na wananchi wengine ambao wamefikwa na kadhia hiyo.
Hata hivyo, maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika yalipigwa marufuku na Jeshi la Polisi, kupitia msemaji wake, David Misime aliyesema hayapo kihalali na atakayeshiriki kwa namna yoyote atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Mbali na Mbowe, wengine waliokamatwa ni Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu, Mwenyekiti Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema na Naibu Katibu Mkuu-Bara, Benson Kigaila.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amedai:”Nilikamatwa juzi saa 12…nikishushwa ndani ya ndege katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere na askari wasiopungua 10.”
Amesema baada ya kushushwa alipandishwa kwenye gari na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege.
Lema alikuwa anatokea Arusha kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA)