Wakuu wa majeshi ya Iran na Saudi Arabia wajadili diplomasia ya ulinzi mjini Tehran

Viongozi wa ngazi ya juu wa majeshi ya Iran na Saudi Arabia wamejadili njia za kuboresha diplomasia ya ulinzi kati ya nchi mbili huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukiendelea kuzidisha mivutano na wasiwasi katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Fayyad bin Hamed al Ruwaili mkuu wa vikosi vya ulinzi wa Saudi Arabia jana Jumapili aliwasili Tehran kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi ya juu wa kijeshi wa Iran. 

Al Ruwaili na Bagheri mjini Tehran 

Katika mazungumzo hayo, Meja Jenerali Mohammad Bagheri Mkuu wa Majeshi ya Iran na al Ruwaili walibadilishana mawazo kuhusu kuboresha ushirikiano wa kiulinzi kati ya pande mbili. 

Bagheri ametilia mkazo umuhimu wa kuboresha ushirikiano wa pande mbili katika nyanja za ulinzi na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na michezo. 

Bagheri  pia ameipongeza Saudi Arabia kwa kuandaa mkutano wa aina yake wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ambao amesema unaweza kuimarisha maelewano kati ya mataifa ya Kiislamu. Mkuu wa Majeshi ya Iran pia amemwalika Waziri wa Ulinzi wa Saudi Arabia kufanya ziara hapa nchini. 

Fayyad bin Hamed al Ruwaili Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Saudi Arabia amesema katika mazungumzo hayo kuwa makubaliano ya Beijing ni fursa ya kimkakati kwa Tehran na Riyadh kuimarisha ushirikiano wa pande mbili. 

Amesema, Iran na Saudi Arabia zina nafasi kubwa katika kuhimiza umoja na mshikamano kati ya Waislamu na nchi za kanda hii na amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano wa kisiasa na kiulinzi kati ya pande mbili.