
Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekutana siku ya Ijumaa jijini Nairobi kujadili hali ya usalama inayoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Mkutano huo uliandaliwa kufuatia agizo la Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (SADC) mapema mwezi huu jijini Dar-es-Salaam, Tanzania. Kabla ya mkutano wa jana, Kikundi Kazi cha Wataalam wa Ulinzi wa EAC kilifanya majadiliano ya siku mbili, kuweka msingi wa mkutano wa leo.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Katibu Mkuu wa EAC Veronica Nduva alisisitiza kuwa Mchakato wa Nairobi ndio njia kuu ya kusaidia serikali ya DRC na raia wake. Huku akikubali changamoto zilizopo, alielezea matumaini yake kuwa amani ya kudumu, usalama na utulivu vinaweza kupatikana kupitia juhudi zinazoendelea kushughulikia vyanzo vya migogoro.
“Jumuiya imejitolea kusuluhisha mzozo Mashariki mwa DRC, na tunawategemea ninyi, wataalamu wa ulinzi na usalama. Nina imani mtatoa hatua zinazohitajika ambazo hatimaye zitaleta suluhu,” Nduva alisema.
Mwenyekiti wa mkutano huo, Jenerali Charles Kahariri, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, alisisitiza udharura wa kushughulikia ghasia na mgogoro wa kibinadamu unaoongezeka nchini DRC. Ametaka mikakati ya pamoja na hatua madhubuti za kukabiliana na hali hiyo.
“Azimio letu la pamoja na moyo wa ushirikiano wakati wa mashauriano haya yanaonyesha nguvu na umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kutafuta amani na utulivu wa kikanda. Ninawapongeza nyote kwa uchambuzi wenu wa kina na mapendekezo yanayotekelezeka, ambayo yameathiri sana maamuzi yetu ya kimkakati,” Jenerali Kahariri alihitimisha.
Mkutano huo uliongozwa na maagizo sita muhimu; Usitishaji mapigano mara moja na bila masharti na usitishaji wa uhasama; Utoaji wa misaada ya kibinadamu; Ufunguzi wa njia kuu za usambazaji; Uundaji wa mpango wa uwekaji dhamana kwa Goma na maeneo jirani; Kufunguliwa tena mara moja kwa Uwanja wa Ndege wa Goma na Ushauri kuhusu afua zingine za uwezeshaji.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa kusainiwa kwa ripoti ya mwisho, ikijumuisha mapendekezo yatakayopelekwa kwenye Baraza la Mawaziri la EAC kwa hatua zaidi.