
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB), Peyman Jebelli, na Mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha IRIB, Ahmad Noroozi wametoa taarifa tofauti wakituba salamu za rambi rambi kufuatia kuuawa shahidi msemaji wa Hizbullah ya Lebanon katika hujuma ya kigaidi ya Israel.
Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, Jebelli amebainisha kuwa kuuawa shahidi Mohammad Afif ni ‘zawadi’ aliyopata kutokana na mapambano yake ya miaka mingi katika uwanja wa vyombo vya habari dhidi ya utawala wa Kizayuni.”
Amempongeza shahidi huyo kwa “kuongoza mapambano ya vyombo vya habari mbele ya utawala wa Kizayuni, na kuchukua jukumu la kufichua jinai za utawala huo ghasibu, hususan zile zilizofanywa wakati wa vita vya hivi karibuni [vya utawala huo] dhidi ya Lebanon.”
Naye Mkuu wa Kitengo cha Kimataifa cha IRIB, Ahmad Noroozi, pia ametoa taarifa ya kumuenzi mkuu wa vyombo vya habari wa Hizbullah aliyeuawa shahidi huku akimpongeza Afif kama “chanzo thabiti na imara” cha kubainisha misimamo ya Hizbullah ya Lebanon.
Noroozi amebainisha kuwa shahidi huyo alikuwaa “kiungo cha mshikamano” kati ya vikundi mbalimbali vya muqawama na vyombo vya habari katika eneo.
Noorozi ambaye pia ni mkurugenzi wa Kanali ya Press TV amesema shahidi huyo alifanya kazi kama “mpiganaji wa njia ya haki na mtetezi wa damu na maisha ya wapiganaji wanaodhulumiwa wa muqawama wanaopambana na utawala katili wa Kizayuni na waitifaki wake.”
Alimsifu Afif kwa usimamizi wake mzuri wa vyombo vya habari, ambao uliambatana na ufahamu wa kina wa kisiasa, ufasaha, nguvu ya ushawishi na ujuzi wa kitaaluma wa uandishi wa habari.
Mohammad Afif, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon aliuawa shahidi Jumapili katika shambulio la kigaidi la utawala wa Kizayuni huko Ras al-Naba, Beirut mji mkuu wa Lebanon.