Wakutubi wafunguka magumu yao, waiangukia serikali

Mwanza. Wahudumu wa maktaba nchini wameeleza changamoto zinazokwamisha maendeleo ya taaluma yao, huku wakiiomba Serikali kuangalia upya kada hiyo.

Wametaja changamoto hizo kuwa ni uhaba wa machapisho, ukosefu wa vitendea kazi, majengo yasiyotosheleza, gharama kubwa za machapisho, upungufu wa ajira na ugumu wa kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.

Wakutubi hao pia wameiomba Serikali kuanzisha maktaba zaidi kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu.

Wamesema hayo leo Jumatatu Novemba 11, 2024 katika kongamano lao linalofanyika jijini Mwanza ambalo litahitimishwa Ijumaa, Novemba 15, 2024.

Agatha Mashilano, mkutubi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) amesema, “tunahitaji uwekezaji katika maktaba kuanzia ngazi za shule za msingi na za jamii, ili kutatua tatizo la uhaba wa machapisho na vifaa.”

Naye Dk Mboni Amiri, mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania, amesema ukosefu wa maktaba umesababisha wahitimu wa kada hiyo kukosa ajira, hivyo kuiomba Serikali itenge bajeti kwa ajili ya ujenzi wa maktaba mpya.

“Tunapenda kuona wakutubi wakiwepo katika shule na vyuo vikuu, ili kuendana na mahitaji ya mitaala ya elimu,” amesema Dk Amiri.

Akizungumzia hilo, Dk Sydney Msonde ambaye ni mwenyekiti wa Muungano wa Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi za Utafiti Tanzania, amesema kuna haja ya kuongeza uwekezaji katika mafunzo na maendeleo ya kitaaluma, ili wahudumu wa maktaba waendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Profesa Peter Msoffe, mkurugenzi wa elimu ya juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, alimwakilisha katibu mkuu wa wizara hiyo, ameahidi kushughulikia changamoto hizo, huku akiwashauri wakutubi kujipambanua kwa ujuzi unaoendana na maendeleo ya teknolojia.

“Tunatambua umuhimu wa maktaba katika kipindi hiki cha mapinduzi ya nne ya viwanda,” amesema Profesa Msoffe.

Kongamano hilo la siku tano linashirikisha wakutubi zaidi ya 150 kutoka mikoa mbalimbali nchini na litahitimishwa kwa uchaguzi wa viongozi wao.