
Mbeya. Chama cha Kutetea Haki na Masilahi ya Walimu Tanzania (Chakamwata) kinatarajia kuwaburuza mahakamani wakurugenzi wa halmashauri 125 nchini sambamba na uongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Hatua hiyo imetajwa ni kushinikiza CWT, kulipa makato ya lazima zaidi ya Sh12.3 bilioni ya wanachama 12,231 nchi nzima.
Katibu Mkuu Taifa wa Chakamwata, Meshack Kapange alisema hayo jana Aprili 8, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho.
Kapange alisema tayari wamepeleka barua za kusudio la kuwapeleka mahakamani na kuwataka kujibu ndani ya siku 30 kuanzia jana Jumanne Aprili 8, 2025.
Alisema wanaowapeleka mahakamani ni wakurugenzi wa halmashauri 125, CWT ambao awali walikuwa wakiwakwepa kujadili masuala yanayohusu masilahi ya walimu lakini sasa wameingia kwenye 18 zao.
“Suala la waajiri kuingilia makato kwenye mshahara ya watumishi bila kuridhia ni makosa chini ya kifungu cha sheria ya ajira na mahusiano kazini cha 28, ambacho kinakataa mwajiri kukata bila ridhaa ya mtumishi husika na akimshtaki faini yake si chini ya Sh1 milioni,” alisema.
Alisema kati ya mikoa yote 26 nchini Mkoa wa Singida pekee hauna changamoto hiyo lakini kwenye halmashauri 125 kinara ni Ilala, Temeke zote za jijini Dar es Salaam na Rungwe Mkoa wa Mbeya.
“Tuna orodha ya mikoa yote na halmashauri ambazo zinadaiwa sambamba na kiwango cha fedha, tumepeleka barua za kusudio la kuwashtaki mahakamani na kutoa muda wa siku 30 wawe tayari wamejibu,” alisema.
Kapange alisema deni hilo lisipolipwa kwa wakati kila mwezi linaongeza kwa zaidi ya Sh222. 3 milioni huku kwa siku litazaa asilimia tano ya riba.
“Tunataka kukomesha tabia ya waajiri kuvamia mishahara ya walimu na katika halmashauri vinara kwa upande wa Temeke ina deni la zaidi ya Sh2.3 bilioni kwa idadi ya wanachama 1,991.
Halmashauri nyingine ni Ilala wanachama 1,771 deni la Sh2.27 bilioni huku kwa Mkoa wa Mbeya ni halmashauri ya Rungwe yenye wanachama 500 na deni la makato ya zaidi ya Sh400 milioni,” alisema.
“Tumetoa maelekezo kwa wanachama nchi nzima kufungua kesi kwa majina ya wakurugenzi wa halmashauri na CWT,” alisema.
Alisema Serikali imekuwa ikifanya vizuri changamoto ni watendaji wa wachache wa ngazi za chini wamekuwa wakitwishwa mzigo sasa wamekuja kivingine: “Na tumesema tabia ya kuvamia mishahara ya walimu ikome.”
“Kazi ni mali ya mwajiri na mshahara ni mali ya mtumishi, tunataka tabia ya kuvamia na kukata mishahara ya watumishi hususani walimu bila idhini yao ikome kabisa,” alisema.
Kauli ya CWT
Kutokana na hilo, Mwananchi limemtafuta Rais wa CWT, Leah Ulaya ambaye alisema chama hicho kimeingia mkataba na Serikali wa kuwatetea walimu wote kwa ujumla.
“Sisi tuna wanachama wengi, na tumeingia makubaliano na Serikali ya kuwatetea walimu, ndio maana wanatakiwa walipe, sio kwamba wanatulipa ada bali ni huduma.
“Kwa mfano hivi karibuni tulikuwa tunawapambania walimu kupandishwa madaraja, Serikali ikiwapandisha, inapandisha wote bila kujali wapo CWT au hawapo,” alisema.
Sababu ya kufikia hatua hiyo
Kwa upande wake, mratibu wa Chakamwata, Mkoa wa Mbeya na Songwe, Anastazius Sanga alisema awali miaka sita iliyopita chama hicho kilisimamishwa kufanya kazi hali iliyosababisha wanachama wao kuingizwa kinguvu CWT, kwa kukatwa asilimia mbili kwenye mishahara yao.
“Hiki ni chama pendwa cha walimu lakini mwaka 2019 tulisimamishwa kufanya kazi ilifunguliwa kesi mahakamani ambapo Februari 27, 2025 walishinda na kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao,” alisema.
Naye Mwalimu Yesaya Kinghomera, alisema tofauti iliyopo ni makato ya watumishi ambapo CWT wanakata asilimia mbili ambayo inalalamikiwa na wanachama.
“Chakamwata wao wanataka asilimia moja kwa wanachama wake, lakini akistaafu anarejeshewa asilimia 50 ya michango yake jambo ambalo linampa mwanga wa namna ya kuanza maisha mapya,” alisema.
Mwalimu Faraja Asheri alisema Chakamwata kimekuwa mkombozi mkubwa kwao na kuomba Serikali kukiunga mkono ili kufikia malengo ya kutengeza Taifa la Tanzania lisilo na malalamiko ya watumishi.
Mmoja wa walimu ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema, asilimia kubwa hawako tayari kujiunga na CWT, lakini wanaingizwa kwa lazima.
“Mishahara yenyewe haitoshi bado makato makubwa kimsingi tunaomba tupewe uhuru, maamuzi yanayofanywa na waajiri ni sawa na kututwisha gunia la misumari na kushindwa kujikwamua kiuchumi,” alisema.