
Dodoma. Wakati maandalizi ya bajeti ya mwaka 2025/26 yakiendelea, wakulima wameiangukia Serikali kuweka ruzuku au kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mifuko ‘kinga njaa’ (hermetic storage bags) kwenye bajeti hiyo, ili kuwaepusha na hasara inayotokana na upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Mfuko mmoja unauzwa kati ya Sh5,000 hadi 5,500, hivyo imekuwa kikwazo kwa wakulima wadogo kumudu gharama za ununuzi na kuwa endapo VAT itaondolewa, bei itashuka hadi Sh3,800.
Wakulima wametoa maoni hayo leo Aprili 4, 2024 kwenye kikao cha usimamizi wa mazao baada ya mavuno ili kuzuia upotevu kwa kutumia mifuko hiyo, kilichoandaliwa na Jukwaa la Wadau wa Kilimo (ANSAF) na Shirika la Ushirikiano la Uswisi linalojulikana kama Helvetas.
Awali, akiwasilisha matokeo ya utafiti uliofanywa kwa ufadhili wa Chuo Kikuu cha Zurich, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Dk Ramadhani Majubwa amesema utafiti umebaini uwepo wa VAT kwenye mifuko hiyo umechangia baadhi ya wakulima kushindwa kutunza mazao yao kwa muda mrefu.
Amesema kuwa changamoto hiyo imefanya wakulima kutokuwa na uhakika wa chakula.
“Utafiti nchini Tanzania kwa wakulima Wilaya ya Kilosa na Kondoa ulibaini kuwa kutoa mifuko ya hermetic kwa wakulima kulipunguza idadi ya kaya zisizo na uhakika wa chakula kwa asilimia 38 wakati wa msimu wa njaa, na asilimia 20 katika mzunguko wa msimu mzima,” amesema.
Profesa Majubwa amesema utafiti uliofanywa na Helvets kwa kushirikiana na ANSAF umeonyesha mahindi yaliyohifadhiwa katika mifuko hiyo hupata uharibifu mdogo au hakuna kabisa. Pia hayana wadudu na unyevu na kutokuwa na sumu kuvu.
Amesema utafiti uliofanywa mkoani Katavi mwaka 2024, ulibaini kuwa upotevu wa mazao wakati wa kuyahifadhi ulipungua kutoka asilimia 40 kati ya mwaka 2015-2018 hadi asilimia 15-20 mwaka 2024.
Akitoa maoni yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mchele, Geofrey Rwiza amesema kwa sasa wafanyabiashara wa mchele wanachokifanya ni kupaka mafuta bidhaa hiyo ili kuepuka kubunguliwa na wadudu.
“Lakini yale mafuta yakikaa muda mrefu yanakuwa si mazuri kwa walaji wa mchele. Kwa hiyo, hapa tunapendekeza mchele tuuweke katika mifuko ya kinga njaa sasa, mifuko hii ni aghali kidogo,” amesema.
Amesema kutokana na ughali wa mifuko hiyo, wafanyabiashara wanaikwepa ili kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuwa wanapendekeza kuondolewa kwa kodi ili iweze kupatikana kwa bei nafuu.
Rwiza amesema kupatikana kwa mifuko huyo kutawahakikishia wakulima na wafanyabiashara kutopata hasara huku afya za walaji zikilindwa.
Amesema mifuko hiyo imekuwa ikiuzwa kati ya Sh5,000 hadi Sh5,500 katika masoko ya Dar es Salaam kwa mfuko mmoja wa kilo 100.
Amesema mchele utakaohifadhiwa kwenye mifuko hiyo ukiwa na unyevu wa asilimia 12.5, unaweza kukaa kwa zaidi ya miaka miwili, huku ukiweka katika gunia la kawaida ukikaa kwa miezi mitatu bila kuharibika.
Meneja Miradi Msaidizi wa Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT), Muhammed Nkya amesema lengo kuhamasisha matumizi ya mifuko hiyo ni kuangalia afya za walaji na uchumi kwa mkulima.
Naye Meneja Masoko wa Kampuni ya Agroz, Obadia Cleophace amesema wadau wamekusanyika jijini Dodoma kwa ajili ya kuiomba Serikali ipunguze ama kuondoa kodi katika mifuko yote ya kuhifadhia mazao, ili mkulima aweze kumudu gharama za upatikanaji wake.
Amesema mradi huo unafanyika katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Katavi na Rukwa.