
Mbeya. Wakulima wa zao la tumbaku, Wilaya ya kitumbaku Chunya Mkoa wa Mbeya wameibua hoja ya kutaka kujua zilipo Sh13 bilioni zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita kama ruzuku kwa ajili ya kuendeleza zao hilo.
Hoja hiyo imeelezwa kuibuliwa na viongozi wa Amcos kwa niaba ya wakulima Jumanne , Machi 24, 2025 kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Chunya (Chutcu), kilicholenga kujadili masuala mbalimbali ya sekta ya kilimo .
Awali ,imeelezwa mapema mwaka jana , Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kutoa ruzuku ya Sh13 bilioni kwa wakulima wa tumbaku nchini jambo ambalo Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe alitekeleza kwa kukabidhi hundi kwa moja ya Taasisi ya masuala ya kilimo Januari mwaka huu.
Akizungumza na Mwananchi Digital Leo Ijumaa Machi 28,2025 , Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Chunya, (Chutcu) Isaya Hussen, amesema mbali wizara husika kukabidhi hundi ya kiasi hicho cha fedha mpaka sasa hakuna mkulima aliyeingiziwa kwenye akaunti kama ilivyo elekezwa.
“Ukimya huo umeibua hofu kwa wakulima kuhoji usalama wa fedha hizo na badala yake kututaka viongozi kutoa majibu sahihi ambapo kwa Wilaya ya Chunya wakulima 8,000 walipaswa kunufaika,” amesema Hussen.
Isaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku (Mtanila Amcos), amesema hali hiyo imesababisha viongozi kunyooshewa vidole na wakulima jambo ambalo sio sahihi.
“Tumemuomba Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka kuingilia kati suala hilo kwa kuwasiliana na waziri mwenye dhamana ya kilimo ili wakulima waweze kupata haki yao ya mgao wa kiasi hicho cha fedha za ruzuku zilizotolewa na serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Awali, wakulima waliwabana viongozi wa Amcos kuwataka kutoa maelezo ya sahihi ya kujitosheleza kuhusu matumizi ya fedha hizo.
“Kumekuwepo na maelezo ya viongozi wa ngazi za juu kueleza kuwepo kwa fedha hizo zilizotolewa ruzuku na serikali cha ajabu hazipo mikononi mwao wala kuingizwa kwenye akaunti za wakulima kama ilivyotarajiwa,” amesema mmoja wa wakulima.
Amesema kuwa kitendo hicho kinaonyesha wazi watendaji wa ngazi za chini wa serikali wanavyoshindwa kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wanyonge.
Mwenyekiti wa Chutcu, Sebastian Masika amekiri kuwepo kwa changamoto ya kutokuwepo kwa taarifa sahihi za fedha hizo za ruzuku kwa wakulima zilizotolewa na serikali.
“Tumewataka wakulima kuwa watulivu kama viongozi tutaendelea kufuatilia kwa viongozi wa kitaifa wenye dhamana ya kusimamia kilimo cha tumbaku kupata maelezo ya Sh13 bilioni zilizotolewa na serikali kwa ajili ya uendelezaji wa zao hilo nchini ,” amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga amesema serikali itaendelea kusimamia sekta ya kilimo kwa kuhakikisha wakulima wanafikiwa na mbolea ya ruzuku ili kufikia tija ya uzalishaji.
“Tutaendelea kusimamia uboreshwaji wa sekta ya kilimo cha tumbaku na kutatua changamoto ili kufikia malengo ya serikali ya awamu ya sita,” amesema.