Wakulima wa tumbaku Shinyanga walalama kuathiriwa na ukame

Shinyanga. Mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na mvua za mawe na ukame mkali, yameathiri uzalishaji wa zao la tumbaku wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, na kusababisha hasara kwa wakulima.

Katika msimu wa kilimo wa 2024/25, zaidi ya ekari 500 za tumbaku zimeathiriwa na hali ya hewa isiyotabirika, ambapo mvua za mawe na ukame zimesababisha kupotea kwa kilogramu 150,000 za tumbaku.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, alizungumza katika mkutano mkuu wa 29 wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU LTD) uliofanyika Machi 22, 2025, ameeleza kwamba chama hicho kilitarajia kuzalisha na kuuza zaidi ya kilogramu milioni 20.3, lakini uzalishaji umefikia kilogramu milioni 15 pekee kutokana na hali mbaya ya hewa.

Mhita amebainisha kwamba KACU LTD ilikuwa na makubaliano na kampuni 11 za ununuzi wa tumbaku, ikijumuisha kilogramu milioni 20 za tumbaku ya mvuke (Fev) na kilogramu 300,000 za tumbaku ya hewa (Burley). Kimsingi, mvua za mawe na ukame vimepunguza uzalishaji kwa kiasi kikubwa, na kuwasababishia wakulima hasara kubwa.

Amesema kuwa wakulima wengi hawana bima za mazao, jambo lililosababisha wengi kushindwa kupata fidia kwa kupoteza mazao yao.

Amewahimiza wakulima na taasisi za kifedha kuwekeza katika elimu kuhusu bima ya mazao ili kusaidia kuondoa hasara kubwa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabianchi. “Kilimo cha mazoea sasa hivi si salama tena. Tuwe tayari kupokea elimu ya bima ya mazao ili kuepuka hasara,” amesema Mhita.

Aidha, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Shinyanga, Kakozi Ibrahim, amewasihi viongozi wa vyama vya ushirika kujiandaa kuendesha shughuli zao kwa njia ya kidijitali na kuzingatia mabadiliko ya tabianchi, ili kuepuka hasara na kuhakikisha wanachama wanafaidika.

Mwenyekiti wa KACU, Emmanuel Nyambi, amezungumzia athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa wakulima wa tumbaku, akionyesha wasiwasi kuhusu ukopaji wa wakulima ambao sasa wamejikuta katika hali ngumu ya kurejesha mikopo yao. “Athari ni kubwa kwa mkulima linapotokea janga kama hujajikinga. Hakika, wakulima wanahitaji kujikinga ili waweze kufidiwa,” amesema Nyambi.

Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Jumanne Kishimba, ameshauri KACU kuongeza mazao mapya yanayoweza kustahimili mabadiliko ya tabianchi ili kusaidia kuongeza wanachama wapya kwenye ushirika, badala ya kutegemea tumbaku na pamba pekee. “Angalieni namna ya kuongeza mazao mapya yasiyokuwa na changamoto nyingi,” amesisitiza Kishimba.

Mkulima wa tumbaku, Zawadi Mashauri, ametoa wito kwa serikali kuongeza uwekezaji katika elimu kwa wakulima wa hali ya chini kuhusu majanga mbalimbali yanayoweza kutokea na mikakati ya kuepuka hasara za kilimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *