
Unguja. Wakulima wa mwani kisiwani Unguja wameeleza ukosefu wa mbegu bora za uzalishaji zao hilo hivyo kurudisha nyuma jitihada zao.
Wakulima hao wameeleza changamoto hiyo jana, Jumamosi Februari 15, 2025, wakati wa hafla ya kukabidhiwa vifaa vya kupandia mwani na ukaguzi wa mashamba darasa ya utafiti wa mbegu bora za mwani katika Pwani Mchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake, Mwanagher Mussa Moh’d amesema mbegu bora ni muhimu kwao ili kuongeza uzalishaji na kipato, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wake.
“Tunashukuru Serikali kwa kutupatia vifaa hivi, lakini bado kuna changamoto ya upatikanaji wa mbegu bora,” amesema.
Kuwepo kwa kituo cha utafiti kisiwani humo kunatarajiwa kusaidia wakulima kulima mwani kwa tija zaidi na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili za Bahari Zanzibar (Zafiri), Dk Zakaria Ramadhan Khamis, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kuandaa bajeti maalumu kwa ajili ya kujenga kituo cha kuzalisha mbegu bora za mwani.
“Ni kweli, miongoni mwa changamoto zinazowakabili wakulima wa mwani ni uhaba wa mbegu bora, jambo linalorudisha nyuma juhudi zao. Serikali imeliona hilo na imetenga fedha kwa ajili ya kuanzisha kituo maalumu cha kuzalisha mbegu bora ili kuongeza thamani ya zao hili,” amesema Dk Zakaria.
Ameongeza kuwa kupitia taasisi ya utafiti, Serikali imeamua kutafuta mbegu bora za mwani unaolimwa nchini ili kuwa na kilimo chenye tija kwa wakulima.
Mwakilishi wa Idara ya Ushirika wa Serikali ya Zanzibar, Haruna Moh’d, amewapongeza wakulima wa mwani kwa juhudi zao za kusarifu bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao hilo, ikiwemo sabuni na mafuta.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wakulima hao kupewa mafunzo juu ya usindikaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na mwani ili kuhakikisha zina ubora wa hali ya juu na kuongeza thamani ya zao hilo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa mwani kutoka Shirika la Good Neighbors, Pius Monchena, amesema shirika hilo kwa kushirikiana na Serikali limekuwa likitoa mafunzo kwa wakulima wa mwani pamoja na kuwapatia vifaa vya kilimo ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji wa zao hilo.