Wakulima wa korosho wavuna Sh880 bilioni, bandari ya Mtwara ikishika hatamu

Mtwara. Wakulima wa korosho nchini wamepata Sh879.699 bilioni katika kipindi cha wiki saba zilizopita, kutokana na mazingira bora ya biashara, ikiwa ni pamoja na uamuzi wa kutumia Bandari ya Mtwara kama lango kuu la kusafirisha zao hilo.

Akizungumza wakati Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, alipotembelea bandari hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, amesema msimu wa 2024/2025 umeanza kwa mafanikio na sasa umefikia wiki ya saba.

“Hadi sasa, uzalishaji na mauzo ya korosho yamefikia tani 261,797 zenye thamani ya Sh999 bilioni na wakulima wamepata Sh879.699 bilioni.

“Tunatarajia kuzidi kiasi cha uzalishaji cha msimu uliopita cha tani 310,000 msimu huu, huku tukiendelea kutumia Bandari ya Mtwara kwa ajili ya kusafirisha. Nimetembelea bandari na kuridhishwa kuwa kuna meli za kutosha kusafirisha korosho za msimu huu,” amesema Alfred.

Aidha, kutokana na uamuzi wa Serikali wa kufanya mauzo ya korosho kupitia jukwaa la Tanzania Mercantile Exchange, hatua ambayo imeondoa madalali waliokuwa wakiwaibia wakulima, wakulima wa zao korosho wamepata bei za juu msimu huu.

Katika mnada wa kwanza uliofanyika Oktoba 11 wa Chama cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu), tani 3,857 za korosho ghafi ziliuzwa kwa bei kati ya Sh4,035 hadi Sh4,120 kwa kilo. Mnada wa pili uliofanyika Oktoba 12 ulioandaliwa na Chama cha Ushirika Lindi Mwamba (LMCU) uliona tani 6,435 zikiuzwa kati ya Sh3,400 na Sh3,865 kwa kilo.

Kanali Sawala amewataka wafanyabiashara wanaonunua korosho mkoani humo kuharakisha mchakato wa kusafirisha mazao hayo kupitia Bandari ya Mtwara, badala ya kuyaacha kwenye maghala kwa miezi mingi.

“Tunatekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo yanalenga kuwafaidisha wakulima, wafanyabiashara na Taifa kwa ujumla,” amesema na kuongeza kuwa ameridhishwa na uendeshaji wa bandari hiyo.

“Tumejionea wenyewe kuwa kuna vifaa vya kutosha za kupakia mizigo kwenye meli. Kwa ufupi, bandari hii inaweza kushughulikia korosho zote zinazokusudiwa kusafirishwa kwenye masoko ya kimataifa msimu huu.”

Kanali Sawala ameipongeza bandari hiyo, akibainisha kuwa ilianza maandalizi ya msimu wa sasa baada ya msimu uliopita kumalizika na sasa inashughulikia hadi tani 500,000 za korosho kwa msimu.

Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi, amesema bandari hiyo ambayo ilisafirisha tani 253,000 za korosho msimu uliopita, imepiga hatua kubwa katika miaka michache iliyopita kwa upande wa kushughulikia mizigo.

“Meli ya mizigo inayoendeshwa na Kampuni ya Mediterranean Shipping Company kwa sasa imeegeshwa katika bandari hiyo ikiwa imebeba kontena 600. Inatarajiwa kuondoka baada ya siku chache, ikipisha meli nyingine kupakia korosho. Tunaendelea kupakia mizigo kwenye kontena ndani na nje ya bandari,” amesema na kuongeza kuwa meli 11 zimehudumiwa tangu msimu uanze.

Nyathi amebainisha kuwa bandari hiyo inaweza kuhudumia hadi tani milioni 2 za mizigo kwa mwaka na kupokea meli zenye urefu wa hadi mita 240. Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa bandari hiyo ilihudumia tani milioni 1.7 za mizigo mwaka jana.

“Itakumbukwa kuwa mheshimiwa Rais aliagiza wakati wa ziara yake mkoani Mtwara kwamba korosho zote zinazovunwa katika mikoa ya kusini zisafirishwe kupitia bandari hii, na tunatekeleza agizo hilo kikamilifu,” amesema.