Wakubwa tujiheshimu mbele ya wadogo

Watanzania kama wanadamu wote duniani tunaheshimu wakubwa. Pamoja na kuaswa kuwaheshimu wakubwa na wadogo, lakini unao usemi wa kimaadili unaokumbusha kuwa aliyetangulia kuliona jua ni mkubwa wetu, hivyo anastahili heshima za kipekee. Yeye amekwisha kupita pale sisi tunapoelekea, na anajua penye changamoto na namna ya kuziepuka kwenye safari. Nyani mzee ni yule aliyekwepa mishale mingi.

Mtoto akifanya makosa huadhibiwa na wakubwa ili asithubutu kuyarudia. Hataachwa ajione kuwa sawa asije akaathirika, lakini pia asije kuwaathiri wengine. Mara nyingi watoto wakidekezwa hukua na makosa yao na kugeuka majambazi, makatili wa kijinsia na kadhalika ukubwani mwao. Wenyewe watajiona kuwa sawa kwani waliachiliwa na jamii kuyatenda hayo tangu utotoni.

Mkubwa anapofanya makosa ni vigumu kumrekebisha tofauti na mtoto. Wanasema “samaki mkunje angali mbichi” kwani akikauka hawezi tena kukunjwa. Ni kwa sababu pengine alikuwa akifanya hivyo tangia enzi hizo kabla wengine hatujazaliwa bila kubugudhiwa. Sasa leo inakuwaje sisi tusiojua lolote tumrekebishe. Ndipo Mheshimiwa anapojibu tuhuma za ubadhirifu kwa kusema, “Nyie mnalalamikia hivi vitone vyenu nilivyojazia pipa langu?”

Chama tawala kinajulikana kuwa kinara juu ya vyama vyote vilivyosalia. Ni mfano wa kifungua mimba aliyewazidi wadogo zake kwa tofauti ya umri wa baba na watoto kwenye familia ya kawaida. Mtoto huyu anaweza kuwatafutia wenzake chakula na kuwalipia ada kwani amekwishaupita utoto, na sasa ni mtu mzima anayewalea wadogo zake.

Tofauti ya chama hiki kikongwe na vyama mahasimu wake kwenye uchaguzi ni ya umri wa mtu mzima. Kina uzoefu wa kutosha kwenye masuala ya uongozi, na wapinzani wake wanalijua hilo.

Lakini hofu inakuja baada ya baadhi ya viongozi wa chama hiki tawala kutumia kauli za vitisho kama kejeli kwa wapinzani. Kauli ya mkubwa inatafsiriwa kama agizo rasmi, hivyo wananchi wanadhani hiyo ndiyo sehemu ya ilani yao ya uongozi.

Ni jambo la aibu kwa chama hiki kinachojinadi kuwa bingwa wa demokrasia nchini kutajwa kuwa kiongozi wa mizengwe ya uchaguzi. Pamoja na wenyewe kuzigomea tuhuma hizi, kila mmoja wetu aliachwa mdomo wazi pale wana CCM wanapokinukisha wakituhumiana wenyewe kwa wenyewe katika kura za maoni. Kwa kawaida wapishi wanaogombania mboga jikoni huwalisha wageni wali mkavu.

Wakati tukisubiri matokeo ya uchaguzi kwenye Serikali za Mitaa, tumeshuhudia vurugu kwenye mitaa mingi zilizowahusisha wanachama wa CCM wakiwafyatukia viongozi wao hadharani.

Waliuona mwenendo wa kura za naoni ndani ya chama chao ukienda isivyo halali. Kwenye Mkoa wa Pwani wanachama waliapa kukipiga chini chama chao baada ya kulazimishwa kuwachagua wagombea wasiofaa kwenye mchakato huo. Huko Mara ndio kumeibuka mengi hususan ya wapiga kura hewa waliotengenezwa na vyama.

Mwananchi mmoja kule Mara alituacha hoi baada ya kudai kuwa mkewe alipotea tangu mwaka 2020, lakini mwananchi huyo akashtuka kuona taarifa za mkewe huyo na jina lake kamili kwenye orodha ya walioandikishwa kupiga kura. Akasema, “Kwa maana hiyo Mtendaji ndiye ataniambia ni wapi alipo mke wangu!” Hii ni hatari sana kwani ugomvi unaweza kuhamia kwenye mahusiano.

Hili linaunganishwa na kuonekana orodha hewa ya waandikishwaji kwenye baadhi ya mitaa. Kwenye Kata ya Bugosi kumedaiwa kuongezwa majina hewa zaidi ya mia tatu baada ya mtu wa mwisho kuandikishwa. Wananchi wengi wamelalamika kuwa wameona majina ya ndugu zao waliokwisha kuondoka huko vijijini muda mrefu kwenda kutafuta maisha mijini. Wengine wamegundulika kuwa chini ya umri, na wengine wagonjwa mahututi.

Sambamba na hilo, vijana wilayani Temeke wanalalamika kutishiwa na wanausalama pale walipojitokeza kwenye zoezi la kuandikishwa tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Walidai wanausalama hao waliwajia na orodha ya viongozi waliopendekezwa kuchaguliwa kinyume na machaguo ya vijana hao. Matatizo kama haya yamekuwa yakijirudia kila mara katika misimu ya uchaguzi.

Dosari za uchaguzi zinaitafuna vibaya nchi ya Msumbiji pamoja na mataifa mengine jirani zetu. Sisi wenye uzoefu mkubwa na uongozi na uchaguzi hatupaswi kuzikopi fujo hizo, bali kujifunza kutokana na makosa ya wenzetu. Kama nilivyotangulia kusema ni aibu kwa wakubwa kutoana macho wenyewe kwa wenyewe mbele za watoto, ndivyo Chama cha Mapinduzi kinatakiwa kutunza heshima yake mbele ya wapinzani wachanga.

Tuendelee kumwomba Mungu atupitishe salama na kutujaza unyenyekevu mbele ya raia wetu. Hawa wakichoka litakuja anguko kuu la amani na utulivu, na hakuna atakayeweza kuyazuia matokeo yake. Tunaambiwa “Kitendo mwana na mjuto ni mjukuu”, tusije tukafika huko kama vipofu wenye shingo ngumu wanaotahadharishwa juu ya mashimo mbele yao lakini wakaishia kumwaga matusi kwa watahadharishaji.