Wakristo wa Armenia nchini Iran: Tuko chini ya Kiongozi Muadhamu katika hali zote

Kaimu Askofu Mkuu wa Wakristo wa Armenia nchini Iran amesema kuwa, wako chini ya amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, katika hali zote.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, matamshi hayo yametolewa na Kasisi Vania Sargiz ambaye ni Kaimu wa Askofu Mkuu wa Wakristo wa Armenia nchini Iran na kusisitiza kuwa, wafuasi wa dini zote humu nchini wataendelea kuwa ni raia wa Iran na amri yoyote inayotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu tutaitekeleza na tutaendelea daima kuwa chini yake. 

Kasisi Sargiz amegusia miongozo ya hivi karibuni ya Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuhusu nguvu za vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, kama alivyosema Kiongozi Muadhamu, vikosi vya ulinzi vya Iran vimeonesha kivitendo nguvu za Jamhuri ya Kiislamu mbele ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kasisi Vania Sargiz

Kiongozi huyo wa kanisa la Armenia nchini Iran amezungumzia pia muqawama wa kupigiwa mfano wa shahid Yahya Sinwar, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na kusema kuwa, shahid Sinwar alikuweko kwenye mstari wa mbele wa mapambano na Wazayuni na kwamba filamu iliyoonesha lahdha na sekunde za mwisho wa uhai wake zimethibitisha jinsi Wazayuni walivyo dhaifu.

Kaimu huyo wa Askofu Mkuu wa Wakristo wa Armenia nchini Iran vilevile amewataja kwa wema mashahidi wote wa njia ya Muqawama na kusema kuwa, walimwengu wanaweza kuchukua kigezo cha umoja na mshikamano wa watu wa dini zote nchini Iran katika kupambana na Wazayuni. Tunamuomba Mungu azipokee dua zetu na auangamize utawala wa Kizayuni.