
WAKATI Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), ikitangazwa kuchezwa mzunguko mmoja, huenda baadhi ya timu kongwe mfumo huo ukazifanya ziwe na wakati mgumu mara itakapoanza.
Ligi hiyo imekuwa ikifanyika katika mizunguko miwili kila mwaka, lakini ile ya mwaka huu itafanyika mzunguko mmoja. Ugumu wa timu hizo unatokana na kasumba ziliyojiwekea ya kucheza vizuri katika mzunguko wa pili, huku zingine zikisubiri nyota wao wafike kutoka wanakoishi.
Timu kongwe ni pamoja na Vijana (City Bulls), Pazi, Savio, Srelio, Mgulani (JKT), KIUT, Chui na DB Oratory.
Kwa mfano timu ya Srelio wachezaji nyota Spocian Ngoma na Joseph Kamamba wanatokea Zambia, Chary Kesseng (Cameroun) na Zadock Emanuel anayetokea Kenya ambapo kwa miaka yote imekuwa ikicheza vizuri katika mzunguko wa pili.
Katika mashindano ya mwaka jana Srelio ilimaliza mzunguko wa kwanza katika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 18 kati ya timu 16 zilizoshiriki. Baada ya kuwasili kwa wachezaji wake wa kigeni katika michezo 20 iliyocheza ilishika nafasi ya nane kwa kuvuna pointi 31 zilizoifanya ikae katika nafasi hiyo hadi mzunguko wa pili ulipomalizika.
Timu nyingine ni Chui ambayo katika michezo ya mzunguko wa kwanza imekuwa na desturi ya kujiweka vizuri, lakini ule wa pili hukomaa zaidi. Chui iliyopambana kujinasua isishuke daraja mwaka jana, katika michezo 20 iliyocheza ilikuwa ya mwisho ikiwa na pointi 23, lakini baada ya hapo ilipanda hadi nafasi ya 12.
Timu zingine kongwe zimekuwa zikibadilishana nafasi katika msimamo wa ligi hiyo kuanzia ile ya saba hadi ya 11.
Akizungumzia mashindano ya mwaka huu, Joseph John, kocha wa kikapu kutoka Temeke alisema ligi hiyo mwaka huu itakuwa na ushindani mkubwa hasa ikizingatiwa kila timu itatafuta nafasi ya kucheza nane bora, ilhali mfumo pia umeshabadilishwa.
PAZI KIMYAKIMYA
Baada ya Pazi kufanya vibaya katika BDL mwaka jana, imeanza kujipanga vizuri kwa ajili ya mashindano ya mwaka huu. Timu hiyo inayofanya mazoezi katika Uwanja wa Tanesco uliopo Msasani, imenasa saini ya nyota watatu wa Mchenga Star na Srelio. Wachezaji hao ni Jovin Ngowi aliyekuwa anachezea Srelio, Ethan na Sam Ogutu waliokuwa Mchenga Stars, ambapo nyota hao ni mafundi wa kufunga katika maeneo yote ya uwanja.
Ngowi anayecheza namba mbili katika nafasi ya shooting guard alilimbia Mwanaspoti kuwa ameamua kurudi nyumbani kuitumikia timu yake ya zamani. “Nimerudi kwa lengo la kushirikina na wachezaji wenzangu kurudisha heshima ya timu iliyopotea,” alisema.