Wakili Lukwago: Kenya ilihusika kukamatwa Kizza Besigye

Wakili wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda amesema kuwa, inaonekana mamlaka za Kenya zilihusika pakubwa katika kukamatwa huko Nairobi Kizza Besigye na kumuondoa nchini kinyume cha sheria.

Wakili Erias Lukwago amesema kuwa, inaonekana kuna amri kutoka serikali ya Kenya katika utekaji nyara wa Besigye hadi kupelekwa kwake kinyume cha sheria nchini Uganda.

Wakili huyo ameeleza kuwa, alipata nyaraka za Besigye kutoka Nairobi licha ya idara ya ujasusi ya Kenya kumkatalia kufika katika chumba cha hoteli ambako Besigye alikaa kabla ya tukio hilo.

Uganda inakabiliwa na ukosoaji wa kimataifa kufuatia kutekwa kutoka mji mkuu wa Kenya kwa kiongozi mkongwe wa upinzani Besigye, ambaye alifikishwa katika mahakama ya Kampala siku ya Jumatano.

Kenya ilisisitiza kuwa haihusiani na kukamatwa kwa kiongozi huyo mwenye miaka 68, ambaye ana taaluma ya daktari wa binadamu na mkosoaji wa muda mrefu wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Kizza Besigye, mwanasiasa mkongwe nchini Uganda Jumatano iliyopita alifikishwa katika Mahakama ya Kijeshi ya Makindye, nchini Uganda. Amerejeshwa rumande hadi Desemba 2.