
Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia wakili wa kujitegemea Qamara Valerian (36) na Benjamin Paul (19) dereva pikipiki (bodaboda) jijini Arusha kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kuvamiwa, kushambuliwa na kumjeruhiwa raia wa kigeni.
Suzan Mary Shawe (75) raia wa Afrika Kusini, alivamiwa na kushambuliwa kisha kujeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili wake na kundi la vijana wenye silaha za jadi Januari 21, 2025 saa 3:00 asubuhi nyumbani kwake Njiro jijini Arusha.
Akizungumzia tukio hilo, leo Januari 25, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo amesema kuwa Januari 21, 2025 Raia huyo (Suzan) alishambuliwa na watu waliotumwa na wakili Qamara kwa nia ya kumtoa kwa nguvu kwenye makazi yake kwa madai ya kutokulipa kodi ya nyumba.
“Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na mara baada ya upelelezi kukamilika taratibu nyingine za kisheria zitafuata,” amesema Kamanda Masejo.
Kamanda Masejo ametumia nafasi hiyo kusisitiza kufuatwa sheria na kanuni katika utekelezaji wa majukumu ya kazi.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari, Suzan alisema juzi Januari 21, mwaka huu, majira ya saa tatu asubuhi akiwa nyumbani kwake, vijana zaidi ya 20 wakiwa na mapanga, nyundo na nondo walimvamia nyumbani na kuanza kumshambulia kwa silaha hizo na kumjeruhi kwa kumpiga nyundo kichwani na kumvunja mkono wa kulia kwa kumpiga na nondo huku wakiwafungia ndani mbwa wake wa ulinzi.
Amesema katika tukio hilo, watu hao pia walimpora simu zake tatu za mkononi pamoja na za wafanyakazi wake na walivamia chumbani kwake na kuiba fedha kiasi cha Shilingi milioni saba pamoja na Dola 2,000 za kimarekani.
“Nilikuwa chumbani kwangu nikasikia kelele, wakati naamka nione dirishani nini kinaendelea ndio dada wa kazi alikuja chumbani kwangu na kuniambia kuna tatizo nje,” amesema Suzan na kuongeza.
“Nilifunga mlango wangu kwa komeo kujihami lakini baada ya muda walikuja na kuvunja mlango wangu wakaingia chumbani kwangu na kunikamata na kuanza kunipiga na nyundo kichwani kisha kuniburuza kutoka ghorofani hadi chini kisha nje ya geti nikiwa mtupu bila nguo,” amesema.
Aliongeza kuwa,”Wakati hayo yote yakiendelea walikuwa wananiambia nitoke ndani ya nyumba kwa sababu nadaiwa kodi wakati nimeishi hapa kwa zaidi ya miaka 20 na marehemu mume wangu aliyefariki miaka miwili iliyopita tukilipa kodi ya mwaka mzima na mwisho nililipa Desemba mwaka jana.”
Amesema kuwa wakati wengine wakiendeleza kipigo hicho wengine waliendelea kupekua chumba chake na kumwaga vitu ambapo waliondoka na simu pamoja na fedha za akiba alizokuwa nazo.
Mmoja wa mfanyakazi wa raia huyo, Ayubu Malolo alisema majira ya saa tatu walifika watu wakiwa na pikipiki sita wakiwa na mapanga na nyundo na kuanza kuwahoji kwa nini wanaishi kwenye nyumba hiyo bila kulipa kodi.
“Sikuwa na jibu nao, ndio wakaelekea kwenye chumba cha bosi wangu, na kuanza kuvunja mlango na kuingia chumbani,” amesema.
“Akaanza kusema ‘mtoeni huyo mzungu’ walianza kumburuza akiwa uchi hadi getini huku wakimpiga na nyundo kichwani, walipofika getini walikuta watu wamejaa ndipo walipomuacha na kukimbia kwa pikipiki zao,” amesema Malolo.