
Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama na wenzake wawili, imekwama kuanza kusikilizwa.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mwandamizi Godfrey Mhini ilikuwa imepangwa kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka leo, Jumatano, Machi 12, 2025.
Kesi hiyo ilipoitwa, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Eva Kasa ameieleza Mahakama kuwa upande wa mashtaka ulikuwa tayari kuendelea na usikilizwaji na kwamba walikuwa na shahidi mmoja.
Hata hivyo, Wakili wa mshtakiwa wa pili na wa tatu, hakuwepo mahakamani na hapakuwa na taarifa zozote kuhusu kutokuwepo kwake mahakamani.
Kutokana na hali hiyo Mahakama imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo, badala yake Hakimu Nyaki ameiahirisha mpaka Aprili 4, mwaka huu kwa ajili ya kuanza usikilizwaji.
Katika kesi hiyo, Mkama na wenzake – Sibuti Nyabuya, aliyekuwa ofisa Tehama wa gereza hilo na Joseph Mpangala, mfanyabiashara mkazi wa Mbezi, wanaokabiliwa na mashtaka manne, ya kuongoza genge la uhalifu, kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa, kuwasilisha nyaraka ya kughushi na kujipatia Sh45 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Wanadaiwa kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa ajili ya wafungwa watatu wenye asili ya China, namba 585/2019 ya Song Lei; namba 205/2019 ya Xiu Fu Jie na 206/2016 ya Haung Quin, waliohukumiwa kifungo katika kesi tofauti zinazohusiana na nyara za Serikali.
Wanadaiwa kuwa Desemba 21, 2022, Mkama na Nyabuya walitengeneza waraka wa kughushi wenye kichwa cha habari ‘’Nyongeza ya Msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru.
Barua hiyo ya Desemba 21 mwaka 2022, iliyodaiwa kusainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya,ilieleza kuwa wafungwa hao watatu wameongezwa katika idadi ya wafungwa waliopewa msamaha na Rais.
Ingawa wafungwa hao walitekeleza sharti la kulipa Sh45 milioni, hawakuwahi kutolewa gerezani humo, hadi mmoja wao alipotembelewa na wakili wake akamwonyesha barua hiyo, ambayo ilipoifuatiliwa ikabainika ni ya kughushi.