Dar es Salaam. Wakili wa upande wa madai katika kesi ya wanafamilia wa John Rupia, Peter Madeleka ameibua jambo baada ya kudai mdaiwa katika kesi hiyo amefanya uharibifu kwenye nyumba inayobishaniwa kinyume na amri ya Mahakama.
Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na John Robert Rupia dhidi ya baba yake mdogo, Stephen Thomas Rupia, kwa madai ya kuingia kijinai katika sehemu ya jengo la urithi wanalolimiliki kwa ubia.
Nyumba hiyo ya ghorofa tatu iliyopo Kariakoo, katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Awali ilikuwa inamilikiwa na John Rupia kabla ya kugawiwa kwa warithi wake watoto wake watatu na familia zao ambao ni Balozi Paul John Rupia na mdaiwa, Stephen, huku kila familia ikimiliki sehemu yake ya nyumba hiyo.
John (mdai katika kesi hiyo) ni mtoto wa Albani John Rupia, hivyo mdaiwa Stephen ambaye ni mtoto wa mwisho wa mpigania uhuru huyo na ambaye alikuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu baba yao ikiwemo nyumba hiyo, ni baba mdogo wa mdai.
Sambamba kesi hiyo ya msingi, pia John amefungua shauri la maombi ya zuio la muda dhidi mdaiwa na wawakilishi au mtu yeyote chini ya maelekezo yake kutofanya jambo lolote katika nyumba hiyo kusubiri kusikilizwa na kuamuriwa kwa kesi hiyo.
Kufuatia maombi hayo, Aprili 14, 2025 mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Lusungu Hemed anayeisikiliza kesi hiyo, ilitoa amri ya upande mmoja ikielekeza nyumba hiyo ibaki kuwa ilivyo mpaka maombi hayo ya zuio yatakaposikilizwa pande zote.
Maombi hayo yalipangwa kusikilizwa leo pande zote lakini yamekwama kutokana na wakili wa mdaiwa Zuri’el Kazungu kutokuwepo mahakamani kwa dharura na badala yake aliwakilishwa na Wakili Sabrina Mhema.
Wakili Sabrina ameieleza Mahakama wakili Kazungu amepata dharura kwa kuwa anahudhuria kesi nyingine Mahakama ya Rufani hivyo anamshikia mikoba tu lakini hana maelekezo yake ya kuendelea na usikilizwaji huo.

Wakili Peter Madeleka, (aliyevaa suti) akiwa nje ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, akizungumza na mteja wake, John Robert Rupia leo Jumatatu Mei 5, 2025.
Wakili Madeleka pamoja na kuhoji uthibitisho wa wakili huyo kuhudhuria kesi nyingine Mahakama ya Rufani akidai kuwa alipaswa kuwasilisha barua kuthibitisha hayo, pia ndipo akaibua madai ya mdaiwa kupuuza amri ya mahakama.
“Mheshimiwa Jaji mara ya mwisho tulipokutana hapa mahakama ilitoa amri ya kudumisha hali ilivyo kuhusiana na nyumba yenye mgogoro, lakini kwa kiburi hiyo amri imevunjwa maana wameanza kuvunja,” amesema wakili Madeleka na kufafanua:
“Mdaiwa ameshatoa milango na madirisha na lengo ni kulifanya jengo lionekane halina thamani waweze kuvunja. Kwa hiyo kama wameshaanza kuvunja maana yake ni kwamba hatuna hata sababu ya kufanya usikilizwaji wa maombi haya pande zote.”
Amesema kama usikilizwaji wa maombi hayo ungefanyika wangeiomba mahakama ikatembelee jengo hilo ili kujiridhisha na madai hayo ya mdaiwa kupuuza amri ya mahakama.
Amesema kama itajiridhisha basi impeleke mdaiwa jela angalau akapumzike kwa miezi sita kwa kosa hilo la kupuuza amri ya mahakama kwa mujibu wa sheria.
“Kwa hiyo kama tungeendelea na usikilizwaji tulikusudia kuleta maombi kwa mdomo ili kuomba mjibu maombi apelekwe jela kwa kupuuza amri ya mahakama maana sheria iko wazi”, amesema Madeleka.
Hata hivyo, Jaji Hemed ambaye amezipokea taarifa hizo bila kuziingiza kwenye mwenendo kutokana na wakili husika wa kesi hiyo kutokuwepo amelekeza upande wa mwombaji kuwasilisha maombi rasmi, kama kuna ukiukwaji huo wa amri ya mahakama siku ya usikilizwaji wa pande zote.
Hivyo Jaji Hemed ameahirisha shauri hilo, mpaka Juni 9, 2025 kwa ajili ya usikilizwaji wa maombi hayo pande zote, tarehe ambayo pia kesi ya msingi imepangwa kutajwa.
Katika kesi ya msingi mdai anaiomba mahakama imuamuru mdaiwa amlipe fidia ya Sh500 milioni kwa madai ya kuingia bila ruhusa kwenye sehemu ya jengo hilo analolimiliki na ndugu zake.
Katika shauri hilo, mdaiwa Stephen (baba mdogo) alikuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu John Rupia ambalo lilimalizika Machi 20, 2025.
Machi 20, 2025 duka namba 5 (ambalo lina asilimia 0.79 ya jengo zima), ghala namba 1 (ambalo lina asilimia 1.33 ya jengo zima), na ghorofa ya kwanza lenye nyumba ya vyumba viwili (ambayo ina asilimia 7.77 ya jengo zima) viligawiwa kwake na ndugu zake.
Juni 24 2024, mdaiwa, bila ridhaa yake mdai aliingia mkataba uitwao “Mkataba wa Uwekezaji” na Mohamed Ali Fakih na Masoud Nassor Hamad, kuhusiana na jengo hilo katika viwanja hivyo ilhali yeye (mdaiwa) siyo mmiliki pekee wa ardhi hiyo yenye mgogoro.
Machi 30 2025, mdaiwa bila ridhaa ya mdai, alijichukulia umiliki na mamlaka ya jumla juu ya mali zote zenye mgogoro zilizotajwa (jengo hilo) na kutoa notisi kwa wapangaji wote waliomo, wakiwemo wa mdai, kuondoka katika jengo hilo kabla au ifikapo Aprili 25,2025.