Wakenya watatu wahukumiwa miezi mitatu jela

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewahukumu raia watatu wa Kenya kulipa faini ya Sh1 milioni kila mmoja au kwenda jela miezi mitatu baada ya kutiwa hatiani kwa makosa la kuingia nchini na kufanya kazi ya ushonaji bila kibali cha ukazi.

Waliohukumiwa ni Selemani Mohamed (23), Sheban Mdune (23) na Hassan Mohamed (26), ambao wote ni mafundi cherehani na wakazi wa Dar es Salaam.

Hukumu imetolewa leo Jumatatu Machi 3, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga baada ya washitakiwa hao kusomewa hoja za awali kisha kukiri makosa yao.

Akiwasomea adhabu hiyo baada ya kukiri, Mwankuga amesema washtakiwa wote anawahukumu kila mmoja kulipa faini ya Sh500,000 kwa kila shtaka au kwenda jela miezi mitatu.

Amesema katika shtaka la kuingia nchini bila kibali, anawahukumu kulipa faini Sh500,000 au kwenda jela miezi mitatu.

Pia, katika shtaka la pili la kufanya kazi ya ushonaji bila kuwa na kibali cha makazi, anawahukumu kulipa faini Sh500,000 au jela miezi mitatu, hivyo kila mshtakiwa atalipa Sh1 milioni au kwenda jela miezi mitatu.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Hadija Masoud ameiomba Mahakama kutoa adhabu kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwao na wengine wenye tabia ya kufanya kazi bila kibali.

Washitakiwa waliomba wapunguziwe adhabu kwa sababu walikuja nchini kutafuta riziki ili kuendesha familia yao.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washtakiwa walitenda kosa hilo Februari 24, 2025 eneo la Kariakoo, Dar es Salaam wakiwa ni raia wa Kenya walikutwa wameingia nchini bila kibali.

Shtaka la pili siku hiyo, washitakiwa wote wakiwa ni mafundi cherehani, walikutwa eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, wakiwa wanafanya biashara ya ushonaji nguo bila kibali cha makazi.