
Moshi.Wakati Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) ikitangaza hali ya mvua na vipindi vya jua katika mkoa wa Kilimanjaro wananachi wa mkoa huo wamelalamikia uwepo wa joto kali nyakati za asubuhi, mchana na jioni hali ambayo imekuwa ni kikwazo kwao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Zaidi joto hilo ambalo linasababishwa na jua kali huwaathiri zaidi watembea kwa miguu, wamachinga na baadhi ya wafanyakazi wa maofisini ambao hawatumii mfumo wa kiyoyozi au feni.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo, Februari 19, 2025 baadhi ya wananchi wa mkoa huo wameeleza namna hali hiyo inavyowapa wakati mgumu hata nyakati za usiku.
Daniela Shao, mmoja wa wakazi wa Wilaya ya Moshi, amesema usiku huwa halali kutokana na joto kuwa kali na kwamba wakati mwingine analazimika kutandika kanga chini ili aweze kupata usingizi.
“Sio mchana sio usiku, ni mateso yaani mchana ukitembea ni kama vile unaskia kama jua limeshuka, usiku nako hatulali joto kali sana, wakati mwingine ukilala unashtuka shuka limelowa, haijawahi kutokea kwa kweli,”amesema Mwananchi huyo.
Mkazi mwingine wa Moshi, ambaye ni machinga, Agusti Swai amesema uwepo wa jua kali unawakosesha raha kwenye kutafuta rizki kutokana na joto na jua kali.
“Yaani unatembea jua kali, unashindwa hata kufanya biashara, kwa mfano sisi watembeza viatu inafika mahali unajificha kwenye kivuli cha mti ili kukwepa jua na joto, kweli ni mateso, sijui nini kimetokea,” amesema mwananchi huyo.