Wakazi Dodoma kupata tiba nyuki bure

Dodoma. Katika kuwawezesha watu wengi kupata tiba nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza kutoa matibabu hayo bure kwa siku tatu jijini Dodoma.

Matibabu ya nyuki yamekuwa maarufu katika siku za karibuni ambapo watu wamekuwa wakitozwa Sh10,000 na kuendelea kwa tiba mara moja.

Akizungumza leo Jumamosi Mei 17, 2025, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana amesema tiba hiyo itatolewa bure katika maonyesho yatakayoanza leo na kuhitimishwa Mei, 20, 2025 wakati wa kilele cha siku ya nyuki duniani.

“Tiba nyuki itakayotolewa bure kwa wananchi watakaotembelea na kuhitaji huduma hii ambayo inasaidia kuimarisha kinga ya mwili,” amesema.

Pia, amesema katika eneo la maonyesho hayo yatakaofanyika kwenye viwanja vya Chinangali II jijini Dodoma, kutakuwa na vivutio mbalimbali vya kitalii wakiwemo wanyamapori hai kama simba, tembo, ndege tausi na wanyama wengine.

Dk Pindi amesema maadhimisho hayo yana lengo la kutambua umuhimu na mchango wa nyuki katika maisha ya mwanadamu.

“Sote tunatambua nyuki na wadudu wengine wachavushaji wanamchango mkubwa sana katika usalama wa chakula, pamoja na uhifadhi bioanuwai,” amesema.

Amesema kati ya wadudu wachavushaji, tafiti zinaonesha nyuki ndiyo wachavushaji mahiri kuliko wadudu wengine.

Ametoa mfano asilimia 80 ya mazao yote ya chakula hutegemea kuchavushwa na mdudu nyuki.

Hata hivyo, Dk Pindi amesema pamoja na umuhimu wake bado mdudu nyuki yuko hatarini kutokana na shughuli za binadamu.

Amesema kupitia maadhimisho hayo yatakwenda kupeleka ujumbe kwa Watanzania na dunia kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kumlinda nyuki pamoja na kutunza mazingira yake.

Amesema kauli mbiu ya siku hiyo ni nyuki kwa uhai na uchumi imara, tuwahifadhi.

Dk Pindi amesema mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo kitakachofanyika Mei 20, 2025 ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Amesema maonyesho hayo yataenda sambamba na matamasha ya nyuki mtaa kwa mtaa.

“Maonyesho yataendelea na kuboresha na Semina muhimu itakayohusu mnyororo wa thamani katika ufugani wa nyuki utakaongozwa na wataalamu wabobezi wa eneo hili kutoka wizarani na wadau wa nje,”amesema.

Amesema Mei 19, 2025, maonyesho hayo yataendelea na wadau watafanya ziara ya mafunzo kenye viwanda vinavyojihusisha na mazao yatokanayo na nyuki.

Naibu Katibu wa wizara hiyo, anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi, Benedict Wakulyamba ametoa wito kwa Wanzania hususan wakazi wa Jiji la Dodoma na mikoa ya jirani kushiriki katika maonyesho hayo.

“Tuungane nasi katika kuadhimisha tukio hili muhimu kwa Taifa letu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *