Wakaguzi wa ndani walia ‘mabosi’ kupuuza ushauri wao

Mwanza. Tabia ya baadhi ya wakuu wa taasisi na mashirika ya Serikali kupuuza mapendekezo ya wakaguzi wa ndani (Internal Auditors) imetajwa kuwa chanzo cha taasisi nyingi za Serikali kupata hati chafu kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka.

Tabia hiyo imebainishwa leo Machi 24, 2025 na rais wa Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani ya Kimataifa nchini Tanzania (IIA), Dk Zelia Njeza wakati wa uzinduzi wa mkutano wa wakaguzi wa ndani unaofanyika kwa siku tano kuanzia leo hadi Machi 28, 2025.

Dk Njeza ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania, amesema wakaguzi wa ndani wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, hata hivyo wamekuwa wakikumbana na vikwazo vya wakuu wa taasisi ama mashirika kutozingatia mapendekezo na ushauri wanaoutoa.

“Kilio chetu kikuu ni miundo kandamizi ya wakaguzi wa ndani mfano muundo wa utoaji taarifa (Reporting structure) wanatakiwa waripoti kwenye bodi au kwa uongozi wa juu jambo ambalo litakalowawezesha kufanya kazi bila kuingiliwa,” amesema.

Ameongeza: “Mkaguzi huyo anatakiwa aripoti katika eneo ambalo hata atakapotoa ripoti yake ripoti yake ichukuliwe na kufanyiwa kazi bila kuathiri utendaji kazi wake, lakini kwa sasa jinsi ilivyo muundo wake ni kandamizi kwa sababu mifumo ya utoaji taarifa sio ya moja kwa moja.”

Akiunga mkono hoja hiyo Mkaguzi wa Ndani kutoka Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, CPA Henry Nyaulingo amesema wakati mwingine mkaguzi wa ndani anaweza kushauri mambo 10 yakafanyiwa kazi mawili, jambo linalosababisha urahisi wa taasisi au shirika kupata hati chafu pindi CAG akija.

“Mkaguzi kazi yake ni kukagua na kushauri viongozi wakuu wa taasisi changamoto ya kimuundo inakuwa ngumu, kwa sababu unakuta kiongozi mkuu wa taasisi ameshikilia masilahi yote ya mkaguzi, hapo anaweza kupokea au asipokee akijua huna cha kumfanya,” amesema.

Akizungumzia changamoto hiyo Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amekiri kupokea changamoto hiyo.

Simbachawene ambaye amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo, amewaagiza Katibu Mkuu Utumishi, Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina kuyachukua na kwenda kuyafanyia kazi ili kuondoa hati chafu kwenye taasisi.

“Madhara ni makubwa ya kutokuwashirikisha hawa wakaguzi kwa sababu ili Serikali ipate kuaminika kwa wananchi ni pale fedha iliyotengwa kwa ajili ya jambo fulani itakapotumika kama ilivyokusudiwa, wakaguzi wa ndani ndio jicho la ndani la taasisi wanapozuiwa kufanya majukumu yao tayari unaanza kupata wasiwasi wa jambo baya linatendeka,” amesema Simbachawene

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *