Dar es Salaam. Usiku wa kwanza unapinduka katika viunga vya Mlimani City, unakofanyika uchaguzi wa nafasi ya uenyekiti wa Chadema na Makamu wake bara na Zanzibar.
Isingekuwa rahisi kwa wajumbe wote kubaki macho baada ya kuvumilia kwa zaidi ya saa 15, wengine wameamua kujilaza.
Kulala sio jambo la ajabu, kinachostaajabisha ni mitindo mbalimbali ya kulala inayoshuhudiwa katika eneo hilo.
Kwa sababu hakuna kitanda, baadhi wamepanga viti vitatu hadi vinne kutokana na urefu wa mtu, angalau kuegesha kupunguza usingizi.
Wapo waliofikwa na usingizi katika viti walivyokalia na kofia walizopewa ndizo wanazotumia kuficha nyuso zao.

Kama ilivyo tabia ya usingizi, hutofautiana kwa kila mtu, wanaokoroma hawakukosekana katika eneo hilo.
Ilikuwa vicheko kwa wengine, lakini kilichoshuhudiwa ni dhahiri kinathibitisha wajumbe wamechoshwa kwa usingizi.
Katika mkutano huo, upigaji kura ulianza rasmi saa 8 usiku na saa 11 zilianza kuhesabiwa.
Kiu ya kujua nani atakayekuwa Mwenyekiti wa Chadema kati ya Freeman Mbowe, Tundu Lissu na Charles Odero ndiyo iliyowaacha macho baadhi ya wajumbe ndani ya ukumbi huo.
Lakini, hata waliolala ni kwa sababu wanataka kuwa sehemu ya mashuhuda wakati mshindi anatangazwa.
Pamoja na kura za wagombea wa uenyekiti, pia zinahesabiwa kura za wagombea wa umakamu uenyekiti bara na Zanzibar.