Wajumbe AAFP wamfyeka mwenyekiti wao mbio za urais

Dar es Salaam. Mkutano Mkuu wa Chama cha Wakulima Tanzania (AAFP), umeibua sintofahamu baada ya wajumbe kumpigia kura za hapana mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Said Soud Said, aliyekuwa akiwania kuteuliwa kugombe urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Mkutano huo ulikuwa na ajenda ya kuwateua wagombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, umefanyika jana Jumanne, Aprili 29 2025.

Kwa upande wa urais wa Muungano, chama kilimteua Kunje Ngombare-Mwiru kuwa mgombea rasmi, huku Chuma Mohamed akichaguliwa kuwa mgombea mwenza.

Kwa Zanzibar, Said alikuwa mgombea pekee, hata hivyo, alikumbana na upinzani baada ya kupigiwa kura 70 za hapana, saba pekee zikimuidhinisha, huku kura nyingine zikiharibika, hivyo nafasi ya mgombea urais Zanzibar ikapangwa kujazwa siku nyingine.

Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo Said aliinuka kwenye kiti chake na kuomba kipaza sauti, alitoa hotuba iliyochukua takriban dakika saba, akieleza kutoridhishwa na matokeo hayo.

Kwa mujibu wa Said anaamini kulikuwa na njama za kisiasa zilizoathiri mchakato huo.

Alidai kuwa, kuna mtu aliyefanya jitihada za makusudi kuwashawishi wajumbe wasimpigie kura, akidai kuwa amefanyiwa ‘uhuni’ ambao hawezi kuufumbia macho wala kuukubali.

Baada ya Said kumaliza hotuba yake, Katibu Mkuu wa AAFP, Rashid Rai aliomba kipaza sauti na kueleza kuwa kutokana na matokeo ya kura, chama hakijaweza kupata mgombea wa urais kwa upande wa Zanzibar.

Alielekeza swali kwa wajumbe, akitaka maoni yao juu ya hatua inayofaa kuchukuliwa.

Rai alimuomba Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, kutoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu hatua zinazowezekana.

Nyahoza aliwashauri kuwa bado kuna fursa ya kumpata mgombea mwingine kupitia mkutano huohuo, mradi waandaliwe kikao kidogo cha ndani kwa ajili ya kujadili jambo hilo kisha kuwasilisha majina mawili ya watakaopigiwa kura.

Baada ya kauli ya Nyahoza, Mwenyekiti Said aliomba tena kipaza sauti na kuwaagiza wajumbe saba aliokuwa ameandamana nao kutoka Zanzibar kuchukua mabegi na mikoba yao, kisha kuelekea kituo cha daladala ili kuwahi usafiri wa kurudi visiwani.

Licha ya jitihada za baadhi ya makada wa chama kumbembeleza asikimbilie uamuzi wa haraka na kumtaka awe mtulivu, wakimkumbusha kuwa maandalizi ya mkutano huo yaligharimu fedha nyingi, Said aligoma.

Kinje Ngombale-Mwiru aliyesimama katikati  mgombea nafasi ya urais   uchaguzi mkuu 2025 kupitia chama cha Wakulima (AAFP)

“Wajumbe hawa ni wake za watu, niliwaomba na niliahidi kwa waume zao kwamba leo hii watarudi kusema, mchakato usogezwe mbele, mnaniweka kwenye mtego ili siku nyingine nisipate wajumbe, wajumbe chukueni mabegi yenu twende tukapande gari tuwahi,” aliwahimiza.

Licha ya juhudi mbalimbali za kumtuliza, Said alionekana kushikilia msimamo wake.

Aliondoka ukumbini kwa msisitizo, huku akipita akitamka kwa sauti maneno yaliyosikika wazi: “Siwezi kuchezewa kihuni kama hivi.”

Said alieleza kwa masikitiko makubwa kutoridhishwa kwake na mchakato wa upigaji kura, akidai kuwa haukuwa huru wala wa haki.

“Haiwezekani hadi watendaji wangu wa chama wenyewe wasinipigie kura. Hilo linaacha maswali mengi ya msingi. Maana yake nini? Kwamba wamepewa pesa?

Kilichofanyika ni uhuni, na ndiyo maana ninafikiria kukata rufaa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuwa,  mchakato huu uligubikwa na vitendo vya rushwa,” alisema Said.

Akiendelea kueleza hisia zake, Said alisema haelewi kwanini wajumbe wote kutoka Zanzibar walimuunga mkono, lakini wale wa upande wa Tanzania Bara, wakiwamo baadhi ya washirika wake wa karibu ndani ya chama, walimpigia kura ya hapana.

“Haiwezekani Wazanzibari wote wanichague, halafu Watanganyika wote wanikatae, tena wakiwamo washikaji wangu ndani ya chama.

“Huu ni uhuni. Naamini rushwa ilitumika, na kuna watu waliingilia kati mchakato wa mkutano ili kunizuia nisigombee nafasi ya urais wa Zanzibar,” alisisitiza.

Said aliongeza kuwa, ana sababu za kuamini kuwa baadhi ya watu ndani ya chama wanahofia uwepo wake katika kinyang’anyiro cha urais wa Zanzibar.

“Kuna hofu. Baadhi yao wanaona nikigombea urais Zanzibar nitakuwa kikwazo kikubwa kwa wagombea wengine, ndiyo maana wanataka kunizuia,” amesema.

“Chama hiki hadi kufikia hatua hii ni nguvu zangu hakuna aliyekuwa anatoa fedha yake mfukoni mimi najitolea zaidi kukijenga chama hiki na huyo anayekuambia sijawahi kununua hata viti nikiwa waziri awamu mbili ni muongo,”alisema.

Alisema baada ya kuzisikia tuhuma hizo tangu juzi aliitisha mkutano wa dharura kuzungumza na viongozi kuondoa kauli hizo ambazo zililenga kumchafua.

“Kile chama nimetumia nguvu zangu kubwa, kuna siri nazijua naweza kuibua na kikafutwa najua kuna makosa gani na gani na nikieleza kupitia vyombo vya habari chama kinaweza kufutwa, nimeshika mpini wa chama hiki,”alisema.

Baada ya kutoka ukumbini, alielekea kwenye daladala pamoja na wajumbe aliokuwa ameandamana nao kutoka Zanzibar, kisha wakaondoka kuelekea Kituo cha Feri kwa ajili ya kurejea visiwani.

Said licha ya kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa zaidi ya miaka 15, pia amewahi kuwa mgombea urais wa Zanzibar mara kadhaa.

Pia, aliwahi kuteuliwa kuwa Waziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), katika baraza la mawaziri lililofanywa na Rais Dk Ali Mohamed Shein ikiwamo kumteua kuwa mmoja wa Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi na Mawaziri Wasiokuwa na Wizara Maalum .​

Said ni kiongozi wa muda mrefu katika siasa za Zanzibar, anayejulikana kwa ushawishi wake katika masuala ya kilimo na haki za wakulima.

 AAFP, chama cha siasa kinachojikita katika masuala ya kilimo, ajira na ustawi wa jamii.​

Mgombea urais Zanzibar

Katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2020, Said alijitosa katika kinyang’anyiro cha urais kupitia tiketi ya AAFP.

Alizindua kampeni zake katika Uwanja wa Ukombozi, Kiuyu Jitenge, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, akiahidi kubadilisha mfumo wa ajira visiwani humo kwa kuondoa upendeleo wa uenyeji na rushwa katika upatikanaji wa ajira.

Pia, alisisitiza kuwa katika Serikali yake, ajira zitatolewa kwa sifa na ufanisi, siyo kwa kujuana au ubaguzi mwingine wowote .​

Mchango wake katika siasa za Zanzibar

Said ameendelea kuwa sauti muhimu katika siasa za Zanzibar, akitetea masilahi ya wakulima na wananchi wa kawaida.

Kwa kupitia AAFP, amekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za kijamii, ajira na maendeleo ya kilimo visiwani humo.

Said amesema uzoefu wake kwenye medani za siasa kumemfanya kujua michezo yote iliyofanyika nyuma ya pazi kumuangusha ili asifanikishe azma yake ya kugombea nafasi hiyo upande wa Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *