Wajue washindi Miss Tanzania tangu 2000, wanachofanya sasa

Dar es Salaam. Mashindano ya Miss Tanzania kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 1967 huku Theresia Shayo akiwa mrembo wa kwanza kutwaa taji hilo, kisha yalisimama kwa muda mrefu na kurejea 1994 ambapo mshindi alikuwa ni Aina Maeda. 

Waliofuatia ni Emily Adolf (1995), Shose Sinare (1996), Saida Kessy (1997), Basilla Mwanukuzi (1998) na Hoyce Temu (1999) ambaye kwa sasa ni Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu katika Mashirika ya Kimataifa Geneva Uswisi. 

Kwa kutambua mchango wao katika tasnia na jamii, tunakuletea makala haya yanayoangazia kwa kina warembo walionyakuwa taji la Miss Tanzania tangu mwaka 2000 hadi 2023 ambapo mashindano hayo yalifanyika kwa mara mwisho. 

1. Jacqueline Ntuyabaliwe 2000

Kabla ya kuwania Miss Tanzania, Jacqueline alikuwa akiimba katika bendi ya Tanzanite tangu mwaka 1997, alishawishiwa kuingia katika ulimbwende ndipo akashinda Miss Ilala kisha Miss Tanzania na kushiriki Miss World iliyofanyika London, Uingereza. 

Baada ya kukabidhi taji nyota yake ilianza kung’aa upande wa Bongofleva akitambulika kama K-Lynn na kutoa albamu mbili, Nalia kwa Furaha (2004) na Crazzy Over You (2007) ila alikuja kuacha muziki baada ya kutoa wimbo wake, She Ain’t a flirt (2009). 

2. Millen Magese 2001

Anatumia ushawishi alioupata kupitia Miss Tanzania kuitumikia jamii yake, mathalani hutoa elimu kuhusu tatizo la Endometriosis ambalo huwafanya wanawake wapate maumivu makali wakati wa hedhi, na pia wasishike ujauzito. 

Julai 2018 Millen alijaliwa mtoto wa kwanza baada ya kusumbuliwa kwa kipindi kirefu na Endometriosis, hiyo ilikuwa ni zaidi ya habari njema kwa wanaofuatilia harakati zake na wahanga wa tatizo hilo. 

                        

Kutokana na harakati zake alipata tuzo ya BET, Music Meets Runway Global Award (MMR), kutajwa kama BBC Unsung Hero 2015 huku 2013 alitajwa na Glitz Africa kuwa miongoni mwa wanawake 20 warembo zaidi Afrika akiwa pekee kutoka Afrika Mashariki.

3. Angela Damas 2002 

Hakupata kuwa maarufu sana kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake, Jacqueline na Millen, mwaka 2014 naye Angela alijitokeza na kutangaza wazi kuwa ni miongoni mwa mamilioni ya wanawake duniani wanaosumbuliwa na tatizo la Endometriosis.

Baada ya kutwaa Miss Tanzania, Angela alishiriki Miss World iliyofanyika hapo Desemba 2002 huko London ingawa awali mashindano hayo yalipangwa kufanyika Abuja, Nigeria ila kwa sababu za ghasia za kidini nchini humo yakahamishiwa London.

4. Sylvia Bahame 2003

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari huko Saudia Arabia, mwaka 2001 Sylvia alirejea nchini na 2002 akajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambako alisomea sheria, akiwa mwaka wa pili chuoni ndipo alipotwaa taji la Miss Tanzania. 

Sylvia ambaye alikuwa mwalimu kwa kipindi kifupi kisha kuingia katika ulimbwende, alihudhuria Miss World iliyofanyika Desemba 2003 huko China, na baada ya mashindano kumalizika alitembelea maeneo kama Hong Kong, Xi’an, Shanghai na Beijing nchini humo. 

5. Faraja Kotta 2004

Alianza kwa kutwaa Miss Ubungo, Miss Kinondoni kisha Miss Tanzania 2004, tangu kukabidhi taji amejikita katika shughuli za kijamii na kwa sasa ni Mkurugenzi wa Shule Direct, jukwaa linatoa mawazo mbadala kukabiliana na changamoto za kielimu kwa wanafunzi. 

Faraja ambaye mwaka 2016 aliteuliwa kuwa  sehemu ya baraza la elimu la World Economic Forum, pia amekuwa akifanya shughuli nyingine za kijamii kama mradi wa ‘Ndoto Hub’ wenye lengo la kuwawezesha vijana wa kike kiuchumi kwa kuwapatia nyenzo muhimu. 

6. Nancy Sumari 2005

Hadi sasa Nancy ndiye mrembo mwenye historia yenye msisimko zaidi tangu kuanzishwa kwa Miss Tanzania, hii ni baada ya kufanikiwa kutwaa taji la Miss World Africa (Continental Queen of Africa) 2005 na ndiye Mtanzania pekee aliyefanya hivyo.

                       

Nancy ambaye 2017 alitajwa katika orodha ya vijana 100 wenye nguvu ya ushawishi Afrika, anatoa mafunzo ya matumizi ya vifaa vya kidijitali kwa watoto kupitia taasisi yake ya Jenga Hub, pia ameandika vitabu vinavyowahusu kama Haki, Nyota Yako n.k. 

7. Wema Sepetu 2006

Anatajwa kuwa mrembo maarufu zaidi katika historia ya Miss Tanzania, baada ya kukabidhi taji, Wema alienda Malaysia aliposomea biashara ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Limkokwing na aliporejea nchini akajitosa katika uigizaji.

Filamu yake ya kwanza kucheza ni A Point of No Return (2007) akiwa na Marehemu Steven Kanumba, kisha zikafuata nyingine kama Family Tears (2008), Red Valentine (2009) na White Maria (2010). 

                       

Wema aliyeshiriki Miss World huko Warsal, Poland, ukiachana na mambo mengi umaarufu wake umekuzwa na uigizaji akishinda tuzo kama Sinema Zetu International Film Festival Award (SZIFF), Hollywood And African Prestigious Awards (HAPAWARDS) n.k. 

8. Richa Adhia 2007

Kwa kiasi fulani ushindi wake uliibua hisia mseto kwa waliokuwa wakifutilia shindano hilo kwa mwaka huo, hii ni kutokana ilikuwa ni mara ya kwanza tangu Miss Tanzania ifufuke mwaka 1994 kwa Mtanzania mwenye asili ya kihindi kunyakua taji hilo. 

Richa alitwaa taji na kuzawadiwa gari aina ya Toyota RAV4 lenye thamani ya Sh45 milioni pamoja na fedha taslimu, vidani na hereni vyenye thamani ya Sh4 milioni, kisha kuiwakilisha Tanzania katika Miss World iliyofanyika Sanya, China hapo Desemba 2007.

9. Nasreen Karim 2008

Alinyakuwa taji la Miss Tanzania akiwa na umri wa miaka 22 akiiwakilisha kanda ya Ziwa, kwa miaka amekuwa akifanya zaidi shughuli za kijamii akiwa kama Mkurugenzi wa Asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Enjipai Masai Women Foundation.

Asasi yake inajishughulika na kazi za utamaduni na sanaa ambazo anawashirikisha kina mama kutoka jamii ya Kimasai lengo kuu likiwa ni kuwainua kina mama hao ambao wanajishughulisha na ubunifu wa shanga kwa kutengeneza vitu vya urembo.

10. Miriam Gerald 2009

Akitokea Mwanza, kanda ya Ziwa, ushindi wa Miriam ulikuja kumaliza utawala wa Dar es Salaam katika mashindano hayo baada ya kupokea taji kutoka kwa mwenzake, Nasreem Karim aliyetokea pia kanda hiyo. 

Alizawadiwa gari aina ya Suzuki Grand Vitara lenye thamani ya Sh53 milioni, fedha taslimu Sh9 milioni, hereni na kidani cha dhahabu kutoka Tanzanite One, pia alichukua na Sh1 milioni baada ya kutwaa taji la mrembo mwenye mvuto kwenye picha, Miss Photogenic.

11. Genevieve Emmanuel 2010

Huyu alianza kwa kutwaa taji la Miss Temeke kisha Miss Tanzania 2010, anakumbukwa kwa kufanikiwa kulirudisha taji la Miss Tanzania jijini Dar es Salaam baada ya mkoa wa Mwanza kulishikilia kwa miaka miwili mfululizo.

Kama ilivyokuwa kwa Miss Tanzania 2000, Jacqueline Ntuyabaliwe au K-Lynn, naye Genevieve aliamua kuingia kwenye muziki na kutoa wimbo wake wa kwanza, Nana (2017) na kupata mapokezi mazuri ingawa sasa haonekani kujikita sana upande huo. 

12. Salha Israel 2011 

Baada ya kumaliza kulitumikia taji, naye aliamua kujikita kwenye tasnia ya uigizaji kama ilivyokuwa kwa Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, Salha filamu yake ya kwanza kucheza ilikwenda kwa jina la Bad Luck (2013) chini ya RJ Company. 

Na katika urembo, alifanikiwa kuingia 30 bora katika mashindano ya urembo (beuty with purpose) ambayo ni sehemu ya Miss World, Beauty With A Purpose, hii uhusisha miradi mbalimbali ya kijamii ambayo hufanywa na washiriki wa Miss World.  

13.  Brigette Alfred 2012

Katika rekodi Brigette ambaye ni Mkurugenzi wa Empowering Margnalised Group, asasi inayowasaidia wenye ualbino, ndiye anatambulika kama Miss Tanzania 2012 ingawa Lisa Jensen ndiye aliiwakilisha nchi katika Miss World huko China.

Ikumbukwe kuwa Lisa alishiriki Miss Tanzania 2006 na kuibuka mshindi wa tatu, huku  Wema Sepetu akitwaa taji na nafasi ya pili ikichukuliwa na Jokate Mwegelo. 

Sasa Lisa aliteuliwa na kamati ya Miss Tanzania kupitia shindano maalumu (Miss World Second Chance) baada ya ratiba ya mashindano hayo ya dunia kubadilika na hivyo kuathiri upatikanaji wa kawaida wa Miss Tanzania. 

14. Happiness Watimanywa 2013 

Alitwaa taji akiwa na umri wa miaka 19 pekee, pia taji la mrembo mwenye mvuto kwenye picha, Miss Photogenic 2013, huku akifanikiwa kuingia mzunguko wa pili katika mashindano ya urembo, beuty with purpose ya Miss World.

Kabla ya Happiness kuwania Miss Tanzania, aliwahi kuwa msichana pekee kutoka Tanzania aliyeweka historia ya kuongoza nchi zaidi ya 150 za mtandao wa IGCSE katika somo la uhasibu kwenye mitihani ya kidato cha nne mwaka 2010.

15. Lilian Kamazima 2014

Anatambulika kama Miss Tanzania 2014 ingawa alikuwa mshindi wa pili, sababu ya kuja kupewa taji baadaye ni kufuatia Sitti Mtemvu aliyeibuka mshindi hapo awali kuachia taji hilo baada ya kubainika kuwa alidanganya kuhusu umri wake.

                        

Ikumbukwe Sitti aliyekuwa pia Miss Temeke aliandamwa na kashfa hiyo hadi kupelekea serikali kuliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kufanya uchunguzi wa sakata hilo na ukweli ulipobainika shindano hilo likafungiwa. 

Sasa Lilian aliyefanikiwa kuingia 10 katika mashindano ya Beauty with Purpose, naye alikuja kuandamwa na tuhuma za mtandaoni kuwa sio raia wa Tanzania, kitu kilichopingwa vikali na wazazi wake lakini ilikuja kubainika hazikuwa na kweli tuhuma hizo. 

16. Diana Edward  2016

Mwaka 2016 shindano la Miss Tanzania lilirejea tena na Diana Edward kutwaa taji hilo, Diana ambaye amekuwa akifanya kampeni ijulikanayo kama Dondosha Wembe ambayo imekuwa ikipiga vita ukeketaji, alikaa na taji hilo kwa miaka miwili.  

Kutokana na hilo, Julitha Kabete aliteuliwa kuiwakilisha Tanzania katika Miss World 2017 huko China. Na kwa upande wake Diana alifanikiwa kuingia fainali ya Beauty With Purpose baada ya kuwasilisha makala ya kupinga ukeketaji kwenye jamii ya wamasai.

17. Queen Elizabeth Makune 2018

Alitwaa Miss Tanzania akiwa na umri wa miaka miaka 22 pekee baada ya kuwabwaga washindani wake 19 alioingia nao fainali, hivyo basi akaiwakilisha nchi katika mashindano ya Miss World 2018 yaliyofanyika huko China. 

Hata hivyo, ikumbukwe kabla ya kutwaa Miss Tanzania, tayari Queen alikuwa ameshinda taji lingine kubwa, nalo ni Miss World University Africa 2017 lililoshirikisha mataifa 53 ya Afrika huko nchini Korea hapo Desemba 2017.

18. Silvia Sebastian 2019 

Mrembo huyo akitokea kanda ya Ziwa, aliiwakilisha Tanzania katika Miss World 2019 huko Uingereza, na aliingia katika 270 bora ya warembo wenye vipaji (Miss World Talent), baada ya kuonesha kipaji cha kucheza robot dance. 

Ikumbukwe mwaka 2020, Silvia alimpokea mgeni wake, Vanessa Ponce De Leon raia wa Mexico aliyekuwa akishikilia tajia la Miss World 2018/19 ambaye aliitembea Tanzania na kuwa mrembo wa kwanza mwenye taji hilo kuja nchini. 

19. Rose Manfere 2020

Alitwaa taji la Miss Tanzania 2020 akiwa na umri wa miaka miaka 21 akiwakilisha kanda ya Dar es Salaam, ushindi wake ulimfanya kuondoka na zawadi ya gari aina ya Toyota Subaru Impreza lenye thamani ya Sh13 milioni.

Hata hivyo, Rose aliondolewa kushiriki Miss World kwa kile kilichoelezwa ni utovu wa nidhamu na nafasi yake kuchukuliwa na mrembo namba mbili, Juliana Rugumisa aliyeiwakilisha Tanzania huko San Juan, Puerto Rico katika shindano hilo. 

20. Halima Kopwe 2022 

Ikumbukwe Miss Tanzania 2021 haikufanyika, hivyo ikarejea tena 2022 na Halima Kopwe aliyekuwa Miss Mtwara kuibuka mshindi na kuzawadiwa gari gari aina ya Mercedes Benz yenye thamani ya Sh40 milioni na kitita cha Sh10 milioni. 

                       

Na utakumbuka kuwa Halima Kopwe alikuwa mshindi wa nne tangu mashindano hayo kuanza kuratibiwa na kampuni ya The Look, washindi wengine ni Queen Elizabeth Makune (2018), Silvia Sebastian (2019) na Rose Manfere (2020). 

21. Tracy Nabukeera 2023

Kati ya warembo 20 waliowania Miss Tanzania 2023, fainali zilizofanyika The Superdome, Masaki, Tracy Nabukeera ndiye aliibuka mshindi katika kinyanganyiro hicho huku naye akizawadia gari aina ya Mercedes Benz na Sh10 milioni. 

Tracy ambaye awali alikuwa akifanya mitindo, ndiye mrembo wa mwisho kushinda Miss Tanzania maana mashindano hayo kwa 2024 hayakufanyika licha ya The Look kutangaza kuwa yapo mbioni na sasa macho yote ni 2025 kuona ni mrembo yupi ataibuka kidedea.