
Dar es Salaam. Wakati wanaume wakiona ni wajibu kutoa zawadi kwa wanawake, wao wanasema hilo linatokana na utamaduni uliojengeka kwa muda, hivyo kuwa kama mazoea.
Mbali ya hilo, baadhi ya wanawake wanasema isiwe mazoea ya kupokea pekee, bali pia nao watoe, huku ikishauriwa zawadi zitolewe kwa nyakati maalumu kama vile katika sherehe za kuzaliwa ili kuonyesha thamani ya upendo.
Hayo wameyaeleza leo Aprili 2, 2025 wakati wakichangia mada kwenye mjadala wa X Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) wenye mada inayohoji: “Kwa nini wanawake hupenda kupewa zawadi wakati wa sikukuu?”
Akichangia mjadala huo, mchangiaji wa Mwananchi X Space, Sadick Hamidu amesema katika kuonesha upendo mwanaume anapaswa kumnunulia zawadi mkewe walau siku za sikukuu, kutokana na yale wanayoyafanya ikiwemo kujitoa kutunza familia.
Amesema kwa asili hata kama mwanamke ana uwezo wa kujinunulia zawadi, lakini atahisi furaha na upendo pale atakaponunulia na mumewe.
“Tuwape zawadi ikiwa ni kuongeza chachu ya upendo katika ndoa kuwapa morali ya kujituma, wanatulindia nyumba na watoto, kwa hiyo hata abaya ya Sh150,000 sioni kama ni kitu kibaya,” amesema.
Pia, Hamidu amesema wanawake nao wanapaswa kuelewa pale mwanaume anapokosa kutoa zawadi, waelewe hali halisi badala ya kuwa nongwa na chanzo cha vita ndani ya nyumba.
Kwa upande wake mwandishi mwandamizi wa habari za kijamii wa MCL, Elizabeth Edward amesema kwa asili mwanamke ameumbwa kupokea hivyo suala la kupenda zawadi kwake ni kawaida.
“Kwa kuwa, kwa asili ameshazoea kupokea, hivyo inapokuja sikukuu kupokea zawadi mfano wa abaya yeye anaona inastahili kuliko mwingine. Zawadi unaweza kupokea kutoka kwa yeyote awe mpenzi, ndugu hata rafiki yako,” amesema.
Amesema kulingana na hali ya maisha ya sasa na ubinadamu unasema ukitaka kupokea na wewe uwe tayari kutoa.
“Unaweza usitoe zawadi, lakini unatoa kujali, upendo, ukarimu, unyenyekevu na wema ikiwa ni malipo ya kile unachopokea. Hili ni suala la kisaikolojia,” amesema Elizabeth.
Naye Mhariri wa jarida la Burudani wa MCL, Christina Joseph naye amezungumzia jinsi mitandao ya kijamii inavyochangia kuchochea mifarakano katikati ya upendo, kutokana na kutoonesha uhalisia wa utolewaji wa zawadi miongoni mwa wapendanao.
Amesema ingawa jamii inaamini mwanamke ni mpokeaji na mwanaume ni mtafutaji hali iliyofanya wanawake kupenda kupokea zawadi, hivyo mwanamke anapoona hajapewa lakini akiangalia mitandaoni akiona wenzake wamepewa anakasirika.
“Mtu anaona hapendwi ndipo ugomvi unapoanza kwa sababu alitarajia hivi halafu mambo yamekuwa hivi, kwa hiyo inaharibu mahusiano na saikolojia ya muhusika,” amesema.
Kutokana na hilo mwanamke anapaswa kuelewa kuna wakati mwanaume anaweza kupata au kukosa, hivyo hata yeye pia anaweza akatoa zawadi.
Kwa upande wake mwandishi wa Mwanchi Digital, Ammar Masimba amesema asili ya wanawake ni sababu ya kupenda kupewa zawadi ingawa kuna wakati baadhi wanakosa kutokana na changamoto za kiuchumi.
“Wanapenda zawadi ni kwa sababu ya asili yao na ni mfumo ambao jamii zetu zimejitengenezea na si vibaya, na si vibaya wanawake kuomba zawadi, lakini lazima wakubali wakipata sawa na wakikosa iwe basi,” amesema
Katika maelezo yake amesema kuna wakati alishawahi kupitia majaribu baada ya kumnunulia mpenzi wake zawadi, lakini sehemu waliyokubaliana kukutana mwenzake hakuonekana.
“Kuna wakati nilinunua zawadi za vitu vya kulakula ili kumpelekea mpenzi wangu kuonyesha upendo, ingawa hakutokea eneo ambalo tulikuwa tumekubaliana na mwisho wa siku nilikula mwenyewe,” amesema.