
Shinyanga. Wajasiriamali wadogo mkoani Shinyanga wameiomba Serikali kuangalia upya masharti yanayotumika kuwapatia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ili kutoa fursa kwa walengwa kunufaika na mikopo hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa licha ya Serikali kuwa na nia njema ya kuwainua wajasiriamali kupitia mikopo hiyo, bado suala la wanakikundi kutakiwa kutoka kwenye eneo moja limeendelea kuwa kikwazo kwa wenye nia ya kukopa.
Wakati mwingine wanaweza kuunda kikundi ndani ya eneo moja, lakini mmoja wa wanakikundi akajiunga kwa lengo la kupata pesa na hana mwamko wa biashara, hivyo kuathiri urejeshaji wa fedha hizo na kuisababishia hasara Serikali.
Evelyne Nnko ni mjasiriamali anayesindika viungo katika manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, alianza na mtaji wa Sh20,000 na sasa ana mtaji wa Sh500,000, amesema baada ya Serikali kusitisha, kuiboresha na kisha kuirejesha mikopo hiyo, ndoto yake ya kukua kibiashara imezimika kutokana na sharti kuwa lazima wanakikundi watoke eneo moja.
Ameiomba Serikali kulitazama upya sharti hilo kwani wakopaji wanaweza kuwa wanaishi tofauti lakini wakawa na lengo moja na wakafanikiwa kurejesha kwa wakati, huku akisisitiza kurejeshwa kwa utaratibu wa kumkopesha mtu mmojammoja.
Amesema amerasimisha biashara yake, amejisajili kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ameongeza thamani bidhaa zake, lakini kupitia biashara hiyo, anasomesha watoto na analipa ushuru wa Sh60,000 kwa mwezi, Sh10,000 anailipa manispaa, Sh50,000 anamlipa mtu aliyemkodishia kibanda sokoni.
“Ila kwa habari ya huu mkopo wa asilimia 10, ambao umetolewa na mama, kweli unatangazwa halmashauri upo, lakini tumeenda halmashauri tumekutana na hii changamoto ya kutakiwa kuwa ni kikundi kinachoishi katika eneo moja,” amesema Nnko.
“Sasa unakuta mimi naishi kata ya Mhungula, nafanya biashara na mwenzangu anaishi kata ya Nyasubi, hatuwezi tukawa kikundi kimoja kwa sababu wametubana na hilo sharti, lakini kata ninayoishi unakuta hawana mwamko wa biashara, ni changamoto kwenye urejeshaji,” ameongeza.
Mratibu wa Mikopo wa Manispaa ya Kahama, Hilda Robert amesema mikopo hiyo inatolewa kwa vikundi kuanzia watu watano, na wote lazima watoke kwenye kata moja ili kurahisisha kamati za mikopo ngazi ya kata kufanya ufuatiliaji wa kikundi husika.
“Mikopo inatolewa kwa vikundi kuanzia watu watano, wawe na katiba, na wawe wanaishi ndani ya kata moja, kwa sababu kwenye kata kuna kamati za maendeleo za kata haiwezi kwenda kumtembelea mtu nje ya kata husika, lakini kwa wenye ulemavu hata mtu mmoja anaweza akakopeshwa,” amesema Robert.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Shinyanga una jumla ya watu milioni 2,241,299, kati ya hao wanawake ni 1,138,420 sawa na asilimia 50.79.
Kwa mwaka 2024/25, Mkoa wa Shinyanga umetenga Sh5.2 Bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu, hadi Februari 2025, Sh2.3 bilioni imetolewa kwa vikundi 19 vya wanawake, 110 vya vijana na 10 vya wenye ulemavu.