Wajasiriamali walia na urasimu, mikopo ya halmashauri ikirejeshwa

Dar es Salaam. Baadhi ya wajasiriamali jijini Dar es Salaam, wameomba kupunguzwa kwa urasimu katika usajili wa vikundi ili kupata mikopo ya halmashauri.

Wamesema hayo huku wakionyesha wasiwasi kuhusu utaratibu wa sasa wa kujisajili kupitia mtandao, wakisema si wote watakaoweza.

Wajasiriamali hao wametoa maoni hayo leo Jumatatu, Novemba 11, 2024 kwenye kongamano la wajasiriamali la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kuelekea kuanza kutolewa tena kwa mikopo ya halmashauri.

Mariam Salum kutoka Buguruni Mnyamani, amesema kumekuwa na mlolongo mrefu wa kuanzisha kikundi, hasa hatua ya kutengeneza katiba na wakati mwingine kuingia gharama kubwa.

“Kuna wakati mama maendeleo ya jamii anakwambia umpe Sh150,000 ili awape wataalamu wakuandikie katiba, ukiwaambia hilo wana kikundi hawakuelewi,” amesema Mariam.

Kuhusu utaratibu wa kujisajili kwa njia ya mtandao, amesema kuna wajasiriamali hawajui kutumia simu janja wala kompyuta, hivyo itawawia vigumu kujaza fomu.

Tiba Lorna, mkazi wa Tabata amesema wakati mikopo ikiwa imerejeshwa ni vema wakachukua vikundi ambavyo tayari vilishaingia kwenye mfumo kabla ya mikopo hiyo kusitishwa mwaka jana.

“Tunaomba vikundi vilivyoingia kwenye mfumo tusiambiwe tena tuanze usajili kwa kuwa tunajua usumbufu wake ni vema kama tayari tuliingia kwenye mfumo basi tuelekezwe hatua za namna ya kupata mkopo,” amesema Tiba.

Leah Mayaya, mkazi wa Tegeta Salasala, ameshauri mikopo hiyo iwe inatolewa na kwa wajasiriamali mmoja mmoja, kwa kuwa wakati mwingine mtu anakosa kuwa na watu wanaofanana kimalengo.

Ofisa Maendeleo Jiji la Dar es Salaam na Mratibu wa Mikopo, Rahma Athuman, akijibu hoja hizo amesema usajili kwa sasa utakuwa bure, na kwa watakaokwama maofisa jamii wapo kuwasaidia.

Kuhusu vikundi vilivyoingia kwenye mfumo, amesema kama wana utambulisho watatambulika ila kutakuwa na uhuwishaji wa taarifa kuendana na utaratibu mpya wa kupata mikopo hiyo.

Kuhusu sifa za kupata mikopo kuna aina tatu ya vikundi vinavyokopesheka ambavyo ni wanawake kuanzia miaka 18 hadi 90 ilimradi ana nguvu kuendelea, vijana kuanzia miaka 18 hadi 45 na wenye ulemavu wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea ilimradi awe ana nguvu.

“Kwa vikundi vya vijana mtapaswa kuanzia watano na kuendelea, mkiwa wanne hamtapata cheti cha utambuzi.

“Kwa wenye ulemavu kuanzia wawili, japo kuna maeneo kama hamna anaweza kukopesheka hata mmoja,” amesema.

Mikopo ambayo itatolewa ni kuanzia Sh5 hadi Sh10 milioni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala, Elihuruma Mabelya amesema kongamano hilo linatolewa baada ya kukamilika kutoa elimu katika ngazi ya kata zote 136, huku wananchi wengi wakionyesha shauku ya kuitaka mikopo hiyo.

“Siku mbili hizi za kongamano zinakwenda kutoa dira zaidi na wajasiriamali watajua mambo mbalimbali, ikiwemo usimamizi wa miradi na namna ya kuiendesha, kusaka masoko na namna ya kufanya marejesho,” amesema.

Awali, akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema halmashauri hiyo ndio imepata fedha nyingi za mkopo kuliko halmashauri nyingine nchini ambazo ni Sh14 bilioni.

Amewataka wajasiriamali kuzichangamkia ili kujikwamua katika umaskini na kueleza inatoa kwa watu ambao si tu wanaishi Ilala, bali wanaofanya biashara katika wilaya hiyo.

“Halmashauri nyingine mikopo inayotolea kwa wanaoishi katika wilaya husika tu, lakini sisi tumekwenda mbali hadi kwa wanaofanya biashara katika wilaya hii, kwani ni eneo ambalo watu milioni tatu wanashinda hapa na watu milioni 1.6 ndio wanaolala usiku,” amesema Mpogolo.