Waitaka Serikali kuunda baraza la lishe kudhibiti upotoshaji

Dar es Salaam. Wadau wa lishe nchini wameitaka Serikali kuanzisha baraza la wataalamu wa lishe litakaloratibu masuala yote ya lishe sambamba na kumaliza tatizo la udumavu kwa watoto wadogo hapa Tanzania.

Wito huo umetolewa leo Aprili 30, 2025 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chama cha Wanataaluma wa Lishe Tanzania (TNDA) Theresia Thomas, lengo likiwa ni kumaliza taarifa potofu zinazotolewa na watu wanaojiita wataalamu wa lishe.

Hitaji la baraza hilo kukabiliana na matatizo ya lishe linakuja wakati ambapo utafiti wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) wa mwaka 2022 umebaini, mtoto mmoja kati ya watatu wenye umri kati ya mwaka 0 hadi mitano wanakabiliwa na tatizo la udumavu wa kimo na akili.

Akizungumza na vyombo vya habari kuhusu jambo hilo, Theresia amesema baraza la lishe litakaloanzishwa litasaidia kudhibiti watu wasio na taalamu ya lishe kutopotosha jamii.

Amesema hivi sasa kuna watu wengi wanaotoa elimu ya lishe na kila mtu anajiita mtaalamu, hivyo kukiwa na baraza litakalosimama kwa mujibu wa sheria, hatua kali zitachuliwa kwa yeyote asiye na taaluma hiyo  kupotosha jamii.

“Kwa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) asilimia 31 ya watoto chini ya miaka mitano wana udumavu, sasa uwepo wa baraza hilo litaangalia kila mkoa mikakati yake ya kupambana na udumavu na kusimamia kupitia kwa wataalamu wa lishe,” amesema.

Amesema baraza litakaloanzishwa litakuwa na nguvu ya kuhakikisha agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, alilolitoa Septemba 2022, akiwataka wakuu wa mikoa kusimamia lishe kwenye maeneo yao, linatekelezwa kwa ufanisi kupitia maofisa lishe.

Theresia ametaja jukumu lingine la baraza hilo kuwa ni kuratibu, kusimamia na kulinda maslahi ya wanataaluma wa lishe na kumaliza changamoto ya utoaji wa taarifa tata kuhusu lishe kwenye jamii.

Pia, amesema kupitia baraza hilo, kampeni mbalimbali za lishe mashuleni zitaanzishwa lengo kuimarisha lishe ya watoto na kuwajengea uelewa umuhimu wa mlo kamili tangu wakiwa shuleni.

Kwa upande wake, Katibu wa TNCDA, Jackson Mathias amesema wataalamu wa lishe wapo katika kila halmashauri nchini, hivyo uwepo wa baraza hilo utasaidia kuimarisha lishe kwenye jamii.

“Takwimu za mfumo wa taarifa za uendeshaji wa huduma za afya (Mtuha) zinaonesha ongezeko la wagonjwa wa NCDs  (magonjwa yasiyo ya kuambukiza) 2,626,107 walitibiwa kwa mwaka 2019 ikilinganishwa na wagonjwa 3,140,067 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la wagonjwa 513,960 au asilimia 20, hivyo baraza likianzishwa litakuwa chachu kuhakikisha elimu sahihi inafika kwenye jamii,” amesema.

Mathias amesema Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha matatizo ya lishe yanakwisha nchini, ndio maana wanaunga mkono juhudi zake na kuiomba Serikali kuanzisha baraza la kuratibu masuala yote ya lishe nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *