Waislamu washerehekea sikukuu ya Eid Al-Adha

Sikukuu hii imeanza kuadhimishwa leo Ijumaa katika baadhi ya mataifa, huku wengine wakingojea kuiadhimisha kesho, Jumamosi.

Karibu Waislamu bilioni 1.9 kote ulimwenguni ambao ni sawa na asilimia 25 ya idadi ya watu, wanasherehekea sikukuu hii ya Eid baada ya kukamilisha ibada ya Hijja mojawapo ya nguzo tano za Uislamu. Na kwenye sikukuu hii Waislamu huandaa kuanzia makazi yao, kununua mavazi mapya na kuandaa vyakula maalumu kabisa kwa ajili ya sikukuu.

Katika siku ya kwanza ya sikukuu hii, wale wanaojiweza kifedha hutakiwa kutoa sadaka ya wanyama ambayo huwa ni kondoo, mbuzi, ng’ombe au ngamia na kuwagawia wasiojiweza sehemu ya sadaka hiyo. Kitendo hicho hurejesha kumbukumbu ya Nabii Ibrahim kumtoa kafara mwanawe wa kiume Ismail kwa utiifu mkubwa kwa Mwenyezi Mungu.

Mambo mengine ambayo hufanyika kwenye siku hii ni kutembeleana, iwe familia ama marafiki, kubadilishana zawadi na kula kwa pamoja.

Lakini ni bahati mbaya kwamba Waislamu kwenye baadhi ya maeneo wanasherehekea sikukuu hii wakiwa kwenye mazingira magumu sana. Huko Ukanda wa Gaza kwa mfano, Wapalestina wa eneo hilo wamelazimika tu kuadhimisha siku hii muhimu kwa Waislamu lakini katika hali ngumu.

Wapalestina wa Ukanda wa Gaza walia na hali ngumu

Waislamu wa hapa Gaza hawana chochote cha kuchinja kwenye sikukuu hii ya kuchinja. Hakuna nyama iliyoingia kwenye eneo hilo kwa miezi mitatu sasa baada ya Israel kuzuia uingizwaji wa vyakula na misaada mingine kwa nia ya kuliongezea mbinyo kundi la Hamas ili liwaachilie mateka wake.

Pakistan Karachi 2025 | Eid al-Adha
Sikukuu ya Idd Al-Adha husherehekewa kwa kuchinja wanyama kama ng’ombePicha: Akhtar Soomro/REUTERS

Na wale kondoo, mbuzi na mifugo mingine iliyokuwa ikifugwa huko Gaza imekufa baada ya vita vilivyodumu kwa miezi 20 sasa kuharibu mfumo wa maisha na iliyosalia ilipigwa mnada. Lakini ni nani aliyeweza kununua mifugo hiyo? Ni wachache tu ndio walikwenda kutazama kondoo ama mbuzi wa kununua, au pengine ng’ombe ama ngamia.

Mkazi mmoja Abdel Rahman Madi alisema hawezi hata kununua mkate, sembuse mbuzi? Si nyama, matunda wala mboga anazoweza kugusa kutokana na gharama kubwa za bidhaa hizo. Ingawa imezoelekea kwenye sherehe kama hii biashara huimarika kutokana na manunuzi kuongezeka, lakini kwa Gaza, mambo ni tofauti kabisa.

Wakazi walalama “Hakuna furaha tena wakati wa Eid”

Nguo kuukuu na vitu vya watoto vya kuchezea vilibaki vimening’inia kwenye mtaa wa soko ulio karibu na mji wa Khan Younis, kutokana na bei kuwa kubwa. Kila mmoja alipita, akatazama, akaenda zake. Mama Hala Abu Nqeira amesema huko nyuma wakati kama huu ulikuwa na shamrashamra nyingi na watoto walikuwa na furaha. Lakini sasa, vizuizi vya Israel vimewafanya wakose unga, nguo na kwa ujumla furaha.

Rasha Abu Souleyman, anasema hivi karibuni alirudi nyumbani kwake huko Rafa alipopakimbia kutokana na mashambulizi, ili angalau achukue chochote kitu kilichosalia. Huko alikuta miwani ya jua, vinguo vichache na bangili alizowapa mabinti zake wawili kama zawadi za Eid. Kwa sasa hawezi kuwanunulia chochote kwa ajili ya sikukuu.

Karima Nejelli, mama na mkimbizi wa ndani kutoka Rafah amesema watu wa Gaza wameadhimisha sikukuu za Eid Al-Adha na Eid El-Fitri mara mbili wakiwa vitani. Na kwenye idd hizo nne wao kama Wapalestina hawakuwa na furaha yoyote. Hawakutoa sadaka, hakuna vyakula, hakuna manunuzi ya nguo, wala chochote kile.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *