Wahujumu SGR kikaangoni, bosi TRC afunguka

Dar es Salaam. Wakati treni ya kisasa ya umeme (SGR) ikitajwa kuwa mkombozi katika kurahisisha usafiri wa haraka kati ya Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma kwa awamu ya kwanza, kumekuwa na changamoto za hitilafu ya umeme inayoathiri ratiba za wasafiri.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema kuna njama zinazofanywa kwa lengo la kuhujumu mradi huo.

Amesema hujuma hizo si za hivi karibuni, bali zimeanza muda mrefu akieleza baadhi ya wahusika wamekamatwa ambao wako mbioni kuchukuliwa hatua.

“Hatua dhidi yao zinaendelea, watakapohukumiwa wananchi watawafahamu,” amesema jana alipozungumza na Mwananchi.

Safari ya kwanza ya treni ya umeme ilianza Juni 14, 2024 kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ikiwa na mabehewa 14 yaliyojaa. Julai 25, 2024 treni hiyo ilianza safari za Dar es Salaam hadi Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan ndiye aliyeizindua.

Mara kadhaa tangu kuanza kwa safari hizo kumekuwa na hitilafu za hapa na pale zinazosababisha adha kwa abiria wanaotumia usafiri huo.

TRC imekuwa na jukumu la kutoa taarifa kueleza kilichotokea na hatua zinazochukuliwa, ikiwemo kuwaomba radhi abiria kwa kuwa mradi huo mpya ndiyo umeanza kutoa huduma kwa mara ya kwanza nchini, hivyo hitilafu ndogondogo hutokea.

Jumatatu ya Novemba 3, 2024, usafiri huo ulipata hitilafu katika mfumo wa uendeshaji, hali iliyosababisha ratiba kuvurugika na abiria kukwama katika stesheni tofauti za SGR.

TRC kupitia taarifa kwa umma iliomba radhi kwa abiria wa treni ya mchongoko (emu) walioanza safari Dar es Salaam kwenda Dodoma saa 2.00 asubuhi na kusimama ghafla saa 2.20 kati ya Pugu na Soga.

Treni ya mchongoko ilikwama ikiwa ni siku ya tatu tangu ianze kufanya kazi ya usafirishaji abiria kati ya Dar es Salaam na Dodoma. Novemba Mosi, 2024, TRC pia iliomba radhi kwa abiria wa treni ya saa 11.15 alfajiri kutoka Dodoma na treni ya saa 3.30 kutoka Dar es Salaam ikijumuisha safari nyingine za siku hiyo.

Siku iliyofuatia, Novemba 4, 2024 treni iliyotoka Dodoma saa 11.15 asubuhi ilikwama kwa dakika 20 kati ya Pugu na Soga.

Mmoja wa abiria aliyepandia Morogoro, amesema ilipofika mbele ya stesheni ya Soga ilisimama kwa zaidi ya dakika mbili hadi tano zilizozoeleka.

Akizungumza na Mwananchi jana kufafanua kuhusu mkwamo huo, Kadogosa amesema kulikuwa na hitilafu ya njia ambayo tayari imerekebishwa na usafiri huo kurudi kwenye shughuli zake kama kawaida.

Amesema kulikuwa na sintofahamu ikiendelea, wengine wakihisi kuna ‘mgawo’ wa umeme kwenye SGR.

“Kuna nyaya zilikatwa kwenye eneo la kati ya Soga na Pugu na waliofanya hivyo si vibaka, ni watu wenye nia ya kuhujumu mradi huu na wanajua walichokuwa wanakifanya.

“Kuna ambao tumeshawakamata na ushahidi upo, na hii si mara ya kwanza, hatukutaka kuwatangaza kwa sababu tulihitaji ‘tu-dili’ nao kimyakimya, hatua dhidi yao zinaendelea na watakapohukumiwa wananchi watawafahamu,” amesema.

Kadogosa amesema hujuma hizo ndizo zimekuwa zikiathiri safari za treni hiyo.

Kwa mujibu wa Kadogosa waya uliokatwa kwenye njia hiyo ni mkubwa na kiufundi hauwezi kukatika hivihivi bali ulikatwa na watu ambao wana utaalamu na ‘mtandao’ na kwamba, wamepambana nao na karibuni watachukuliwa hatua stahiki.

Amesema eneo ambalo nyaya za njia ya reli zilikatwa ni baada ya stesheni ya Soga kwenda stesheni ya Pugu.

“Hii siyo mara ya kwanza, tulichokibaini wanaofanya vitu vyote hivyo wanataka kuwepo na kelele ili mradi uonekane haufai, lakini tutapambana nao, kuna muda madereva na mainjinia wetu wanasakamwa, lakini vinavyotokea hata wao vipo nje ya uwezo wao. Hawa watu wanafanya vitu hatari sana, zile nyaya zina high voltage (umeme mkubwa), ukizigusa unakaukia pale, tutapambana nao kwani, ushahidi tunao,” amesema.

Kuhusu treni mchongoko kupata hitilafu, Kadogosa amesema kati ya treni tatu walizonazo (Magufuli, Samia na Nyerere) hakuna hata moja mbovu.

“Kuna video zilikuwa zinasambaa kwamba mchongoko ni mbovu, lakini si kweli, kwenye mchongoko ni ishu ya ‘technical replace’, kubadilisha vichwa, hakuna hata moja iliyopata hitilafu, tatizo tulilokuwa nalo ni njia,” amesema.

Kuhusu suala la hujuma, mbali ya Kadogosa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima kwa nyakati tofauti waliwahi kueleza namna mradi huo unavyohujumiwa na baadhi ya watu.

Julai 6, 2024 Malima alieleza kukamatwa kwa watu watatu kwa tuhuma za wizi na uharibifu wa miundombinu ya reli hiyo kipande cha Morogoro-Dodoma.

Agosti 15, Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Morogoro, Christopher Mwakajinga amesema baadhi ya abiria wanalipa nauli kidogo. Alieleza waliopaswa kushukia vituo vya Pugu, Ruvu na Ngerengere hawateremki katika vituo hivyo, badala yake wanakwenda hadi stesheni ya Morogoro.

Mchumi ashauri

Mchambuzi wa masuala ya uchumi nchini, Oscar Mkude amesema mbali na changamoto hizo ambazo katika maisha ya kawaida hutokea, TRC inapaswa kubadilika katika mfumo wake wa utoaji taarifa.

“Hata kama wamekosea, kutoa taarifa ndiyo uungwana ukizingatia usafiri huu unapendwa na wengi, wakiwamo waliotoka kwenye mabasi au ndege na kuhamia huko. Changamoto huwa zipo na ilipoanza hata wananchi tulizitarajia na hata kwenye ndege zinatokea, lakini ukitoa taarifa unampa mtu nafasi ya kujipanga, pia ni vema ikawapa abiria mbadala wa usafiri.”