Moshi. Wahamiaji haramu 35 raia wa Ethiopia na Burundi wamekamatwa Mkoa wa Kilimanjaro wakitumia njia za panya (njia zisizo rasmi) kuingia nchini Tanzania kinyume cha sheria.
Wahamiaji hao wamekamatwa Mei 10 na Mei 15, 2025 katika Kijiji cha Mji Mpya kata ya Mabogini, Wilaya ya Moshi mkoani humo baada ya maofisa wa Uhamiaji kupata taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu uwepo wa watu hao katika eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi, Mei 17, 2025, Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Augustino Malembo amesema raia hao walikamatwa wakiwa wamejificha katika shamba la mahindi katika Kijiji cha Mji Mpya.

Mkuu wa uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Augustino Malembo akionyesha baadhi ya wahamiaji haramu waliokamatwa.
Malembo amesema wahamiaji hao 33 ni raia wa nchini Ethiopia na wawili ni raia wa Burundi na kwamba taratibu nyingine za kisheria zinaendelea dhidi yao.
“Baada ya kuwahoji tumejiridhisha watu hao ni wahamiaji haramu kwa kuwa hawakuwa na nyaraka zozote za kusafiria na hawakupita katika vituo rasmi vya kuingilia nchini na walikuwa wakipita kuelekea Afrika Kusini,” amesema Malembo.
“Lakini pia tunaendelea na uchunguzi ili kujua watu waliohusika kuwasaidia wahamiaji hao kuingia nchini ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao,” amesema.
Aidha amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi hususani viongozi wa ngazi ya chini ili waweze kutoa ushirikiano pindi wanapowaona wahamiaji haramu wanaoingia nchini bila kufuata utaratibu na kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe kwa haraka.
“Elimu kuhusu mjue jirani yako inaendelea kutolewa na Maofisa uhamiaji kata kwa wananchi hususani maeneo ya mipakani ili kuweza kufahamu wageni wanaoingia na kufanikisha jitihada za kudhibiti wahamiaji haramu kuingia nchini bila kufuata utaratibu,” amesema.
Akizungumzia kuhusu changamoto ya wahamiaji haramu nchini, Joyce John, mkazi wa Moshi amesema ili kuweza kudhibiti wahamiaji haramu, elimu kwa kina inapaswa kutolewa kwa wananchi hususani wa mipakani, ili kuweza kuwazuia kabla ya kuingia nchini.
“Wahamiaji haramu hawa wanapita maeneo ya mipakani ambako kuna watu, watu hawa wanapaswa kuelimishwa madhara ya kukaribisha watu wasiowafahamu ili wote wawe na uelewa na kushiriki kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu kuingia nchini,” amesema.
Kuanzia Januari hadi Mei 15, 2025, wahamiaji haramu 65 wamekamatwa katika maeneo tofauti mkoani Kilimanjaro, kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria.