Ndege iliyokuwa imewabeba wahamiaji 199 waliofukuzwa nchini Marekani imewasili nchini Venezuela.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Akithibitisha kuwasili kwa raia hao, Waziri wa usalama wa ndani wa taifa hilo Diosdado Cabello amesisitiza kwamba wako tayari kuwapokea raia wake kutoka popote walipo.
Picha za moja kwa moja zimeonyesha vijana wenye umri mdogo wakishuka kutoka kwenye ndege ambayo ilitua katika Mji mkuu wa Caracas.
Baadhi yao kulingana na picha hizo walikuwa wakipiga makofi wakati wakishuka kutoka kwenye ndege huku wakisubiriwa na maofisa kwenye taifa hilo.
Wahamiaji hao wamerejeshwa nyumbani baada ya nchi yao Jumamosi ya wiki iliopita kutangaza kwamba ilikuwa imefikia makubaliano na Washington kuhusu kurejelewa kwa safari za ndege za kuwaondoa raia wa Venezuela kutoka Marekani.
Zoezi la kuwaondoa raia hao lilikuwa lilisitishwa mwezi uliopita wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipodai kwamba Venezuela haijatimiza makubaliano ya kupokea haraka wahamiaji waliofukuzwa Caracas kwa upande wake ikisisitiza kwamba haitakubali tena ndege hizo za wahamiaji.