Moshi. Wakati Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) ikihudumia wagonjwa wa saratani zaidi ya 9,000 kwa mwaka, imesema wagonjwa wapya 900, ambao huongezeka kila mwaka sawa na asilimia 65, wanahitaji tiba ya mionzi.
Hayo yameelezwa jana, Jumamosi, Machi mosi, 2025, na Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Profesa Gileard Masenga, wakati akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa jengo la tiba na mionzi kwa wagonjwa wa saratani linalojengwa hospitalini hapo kwa Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, alipolitembelea jengo hilo.
Profesa Masenga amesema jengo hilo, ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 94, linatarajia kugharimu Sh16 bilioni hadi kukamilika kwake, ambapo huduma hiyo itaanza kutolewa Juni 2025.
“Idara ya Saratani inahudumia wastani wa wagonjwa 9,446 kwa mwaka hapa KCMC na wagonjwa 900 wapya kila mwaka, ambapo kati yao asilimia 65 wanahitaji tiba ya mionzi, hivyo hulazimika kusafiri kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya mionzi Ocean Road,” amesema Profesa Masenga.

Ameeleza kuwa mradi huo umelenga kutoa huduma kwa wagonjwa wa saratani wa Kanda ya Kaskazini na nje ya Mkoa wa Kilimanjaro, na hivyo kupunguza gharama za kusafiri kwenda kutafuta huduma hiyo jijini Dar es Salaam.
Aidha, Profesa Masenga ameishukuru Serikali kwa kutoa Sh3 bilioni kwa ajili ya gharama za ujenzi wa jengo hilo, akisema kukamilika kwake kutapunguza adha kwa wananchi.
“Tunashukuru uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa mradi huu. Tunategemea mwishoni mwa mwezi wa nne uwe umekamilika, na mwisho wa mwezi Mei tutakuwa tayari kutoa huduma,” amesema Profesa Masenga.
Akizungumza baada ya kutembelea jengo hilo, Waziri Mhagama amesema mradi huo utapunguza mzigo kwa wananchi ambao wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za kibingwa na kibobezi Ocean Road.
Amesema ongezeko la wagonjwa wapya wa saratani 900 kila mwaka KCMC si idadi ndogo na kwamba jitihada zaidi za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza zinahitajika.
“Ni lazima tuanze kampeni ya hali ya juu ya kuelimishana ili watu watambue kuwa magonjwa haya yasiyoambukiza ni magonjwa ya muda mrefu, matibabu yake yanatumia fedha nyingi, lakini pia yanahitaji uwekezaji mkubwa ili huduma hizi ziweze kutolewa kadri inavyowezekana,” amesema.
Waziri Mhagama amesema magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, na matatizo ya figo yameendelea kuongezeka hapa nchini, hivyo amewataka wananchi kuchukua tahadhari zote.
“Magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kuongezeka kwa kasi hapa nchini, ni magonjwa makubwa na matibabu yake yanahitaji ubobezi wa hali ya juu. Bila kuwa na madaktari wabobezi hatuwezi kutibu wagonjwa kama wa saratani, figo na moyo,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa kutoa Sh8.9 trilioni kwa ajili ya uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya majengo na vifaa tiba katika sekta ya afya hapa nchini.