Wagonjwa wa TB hatarini baada ya ufadhili wa USAID kusitishwa

Shirika la afya duniani WHO, linasema uamuzi wa utawala wa rais Donald Trump, kusitisha msaada wa kigeni utarudisha nyuma hatua zilizopigwa katika kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB) katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa yake, WHO inasema hatua hii ya Marekani itaweka maisha ya mamilioni ya raia kwenye nchi masikini kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa ugonjwa huu.

Dr Tereza Kasaeva, mkurugenzi wa Mpango wa Kimataifa wa WHO kuhusu Kifua Kikuu na Afya ya Mapafu, anasema ‘Bila hatua za haraka, maendeleo yaliyopatikana katika vita dhidi ya TB yako hatarini’.

Misaada muhimu ya kimataifa, hasa kutoka kwa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), ilisaidia kuepusha takriban vifo milioni 3.65 mwaka jana pekee kutokana na ugonjwa huo hatari, ilisema taarifa ya WHO.

Mataifa maskini duniani yamekuwa yakitegemea pakubwa msaada kutoka kwa shirika la USAID.
Mataifa maskini duniani yamekuwa yakitegemea pakubwa msaada kutoka kwa shirika la USAID. REUTERS – Kent Nishimura

Kihistoria Marekani imekuwa ikichangia karibi moja ya tatu ya jumla ya ufadhili wa kimataifa kwa ajili ya programu za TB, ambayo ni sawa na dola milioni 200 hadi milioni 250 kila mwaka.

Hatua ya Marekani, unaziweka nchi 18 zenye idadi kubwa ya maambukizi ya TB katika hatari, huku eneo la Afrika likiwa limeathirika zaidi.