Wagombea umakamu mwenyekiti Chadema waja na hoja ya mabadiliko

Dar es Salaam. Wagombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar na Tanzania Bara, wamesema chama hicho kinahitaji mabadiliko ya kweli ili kuuaminisha umma katika kupigania haki zao za msingi.

Hoja ya mabadiliko imetajwa na wagombea hao  kwa nyakati tofauti wakati wakijieza katika kuomba kura kwa wajumbe wakisema sasa Chadema kinahitaji kiongozi ambaye akisema jambo linatekelezeka kama alivyoahidi.

Katika hatua nyingine wagombea hao upande wa Zanzibar wameibua hoja ya Chadema visiwani humo kimelala  na kinahitaji kiongozi atakayekiamsha kwa kufanya mikutano ya hadhara mara kwa mara kama inavyofanyika Bara.

Usingizi wa Chadema upande wa Zanzibar ndio uliowafanya wagombea  wanne wa nafasi hiyo kutukia turufu hiyo kushawishi wajumbe  kuwapa imani kwa kwenda kubadili taswira ya chama hicho.

Kwa upande wa wagombea Tanzania Bara, nao wameendeleza hoja hiyo wakieleza wanachama wamekuwa na makovu ambayo baada ya uchaguzi  yanahitaji tiba ili kurudisha nguvu ya umoja.

Hoja nyingine ni suala la rushwa ambalo bado limeendelea  kuwa mwiba kwa chama hicho kwani baadhi ya wagombea wamedai bado harufu yake ndani ya uchaguzi wa chama ipo hivyo anahitajika kiongozi ambaye atakuwa sauti na mwenye kukibadili sura ya chama hicho.

Hoja za wagombea

Mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar Hafidhi Ali Saleh akiomba kura kwa wajumbe na kujieleza amesema anaomba nafasi hiyo kukinyanyua chama hicho.

“Chama chetu kimekuwa kama kilema kinahitaji kunyanyuliwa kwa upande Zanzibar, nimeingia kwenye kinyanganyiro hicho baada ya kuona wivu Chadema bara ni imara na Zanzibar inasuasua,”amesema.

Amesema ameamua kugombea nafasi hiyo kushiriki upatikanaji wa Serikali upande wa Zanzibar na katiba mpya akieleza anauwezo wa kuendesha Kanda ya Unguja na Pemba.

Kuhusu mkakati wa kujenga chama hicho ikiwa ni swali la wajumbe,Salehe amesema atahakikisha kanda zote zinafanya uchaguzi na kukamilisha pamoja na kuongeza idadi ya wanachama ambao sasa wanakihitaji chama hicho.

Mgombea mwingine wa nafasi hiyo ambaye pia anatetea kiti hicho Said Issa Mohammed, amewaomba wajumbe wamchague ili akakamilishe maono yaliyobakia ya kushika dola.

“Nilianza kazi ya kusimamisha wagombea kwa nafasi ya madiwani, wabunge na wawakilishi, lakini hata hivyo kutokana na changamoto zilizojitokeza tukishinda viti vitatu tu,” amesema

Wakati mgombea huyo akijieleza alalizimika kusimamisha hotuba yake kwa dakika takribani mbili baada ya kutokea kwa mabishano baina ya wajumbe na baada ya muda mgombea aliendelea kujinadi.

Katika kuendelezo wa kujinadi Mohammed amesema shabaha yake ni kukahikisha Chama hicho kinapata fursa yakuingia kwenye serikali ya umoja wa Kitaifa.

“Nipo tayari kukitumikia chama hiki muda wowote na uzuri afya yangu imeimarika tofauti na mwaka 2020 nilipitia hali ngumu kwanza nilifiwa na mke wangu lakini niliumwa na nikifanyiwa operesheni mara mbili,” amesema.

Mwingine aliyeomba ridhaa ya kuongoza Chadema kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Zanzibar Said Mzee Said ameomba kupewa ridhaa hiyo akiahidi kuleta mabadiliko ambayo yanahitajika Zanzibar.

Amesema rekodi ambayo Chadema imewahi kuweka kuwa na wabunge wengi na madiwani haijawahi kuvunjwa kitendo ambacho kimeififisha chama hicho.

Said katika kujinadi kwake ametupa dongo kwa makamu mwenyekiti aliyemaliza muda wake hakuwa akifanya shughuli za kukikuza chama hicho.

Mgombea mwingine ni Suleiman Makame Issa aliyesema wanahitaji mabadiliko ili kukisukuma chama hicho kwa kuwa siasa za upinzani zimepoa kwa sasa.

Kwa sababu ana uzoefu wa zaidi ya miaka 30 ya utumishi wa umma, amesema anatosha kukiongoza chama hicho kwa nafasi ya Makamu Zanzibar.

Alipoulizwa swali kuhusu nini falsafa ya Chadema, amejibu ni Stronger Together na kuibua vicheko kutoka kwa wajumbe.

Vicheko hivyo vimetokana na mgombea huyo kukosea majibu, badala ya kusema nguvu ya umma amejibu strong together.

Wagombea bara

Kwa upande wake, mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Ezekia Wenje amesema safari ya ukombozi iliyoanzishwa na waasisi wa chama hicho bado inaendelea, hivyo achaguliwe akaendeleze mapambano.

“Pamoja na wasifu wangu wa nafasi mbalimbali ya kuongoza kamati tofauti lakini natambua bado kuna kazi kubwa ya kufanya na kuna waliowengi wanamakovu kwa sababu ya kupigania haki ya nchini hii,” amesema.

Wenje amesema moja ya majukumu ya nafasi anayoiomba ni kumsaidia mwenyekiti wa chama na mwenyekiti wa kamati ya maadili pia anaamini kupitia uzoefu alionao ataweza kutekeleza majukumu kwa weledi.

“Najua kuna changamoto kubwa ikiwemo chama chetu kinatakiwa kuwa na uwezo wa kujiendesha ilibkuendeleza mapambano ya kudai haki za wananchi,” amesema

Amesema anafahamu ili waweze kufanya jambo lolote wanahitaji raslimali fedha hivyo akifanikiwa kuchaguliwa katika nafasi hiyo atatafuta vyanzo vya kujiingizia kipato.

“Hatuwezi kukaa tusubirie ruzuku pekee katika kukiendesha chama nikipata madaraka nitatumia nguvu zangu zote kutafuta na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato,” amesema

Kuhusu mbinu atakayotumia kuponya makovu yatokanayo na uchaguzi Wenje amesema atawafikia watu wote na kuongea nao kujenga muafaka kwakuwa wanachama wote wanahitajihana.

Naye mgombea wa nafasi wa makamu uenyekiti bara, John Heche amesema anagombea nafasi hiyo katika kipindi ambacho kunahitajika watu wa kubadilisha nchi.

Amesema wanahitaji wanasiasa watakaojibizana na washindani wao na watakaosimama kiasi kwamba sura ya Chadema inaonekana.

Amesema anahitajika mtu anayejua madhumuni na malengo ya kuanzishwa kwa Chadema.

Amesema anahitajika Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili atakayekemea rushwa bila woga.

Amesema wanahitajika watu watakaoweza kushusha ruzuku hadi chini ili angalau viongozi wa chini waweke mafuta walau kwenye pikipiki ili wakafanye kazi ngazi ya chini.

Kwa mujibu wa Heche, mtu huyo atakayeweza kuyafanya yote hayo ni yeye kutokana na uwezo wake.

Naye Mgombea wa nafasi hiyo, Mathayo Gekul ameomba kuaminiwa na wajumbe kukiongoza chama hicho kuanza kusimamia mabadiliko ndani ya chama na nje ya chama.