Wagombea 18 kuchuana urais CWT, 19 umakamu

Wagombea 18 kuchuana urais CWT, 19 umakamu

Dar es Salaam. Jumla ya wagombea 37 wanatarajiwa kushindania nafasi za Rais na Makamu wa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Mei 28 na 29, 2025, jijini Dodoma.

Kati ya wagombea waliojitokeza, 18 wanawania nafasi ya urais huku 19 wakigombea nafasi ya Makamu wa Rais. Makamu wa Rais wa sasa, Ikomba Suleiman, amejiunga katika kinyang’anyiro cha urais na atapambana na Rais aliyepo madarakani, Leah Ulaya, ambaye anawania kutetea nafasi hiyo.

Jina la Leah lilivuma mwaka juzi baada ya Januari 25, 2023 kukataa uteuzi wa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbongwe, mkoani Geita, aliopewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Pia, aliyekuwa Katibu wa CWT, Japheth Maganga, pia alikataa uteuzi wa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera huku aliyekuwa Makamu wa Rais wa CWT kwa kipindi hicho, Dinah Mathamani, alikubali uteuzi na akaenda katika Wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma.

Uchaguzi huu unatarajiwa kufanyika baada ya kukamilika kwa uchaguzi katika ngazi mbalimbali nchini za chama hicho, kuanzia ngazi za shule (Tawi), wilaya na mikoa. Sasa, chama kinajiandaa kumalizia mchakato wa uchaguzi katika ngazi ya Taifa.

Nafasi nyingine zinazotarajiwa kufanyiwa uchaguzi ni pamoja na katibu mkuu wa CWT, naibu katibu mkuu, mweka hazina, mwakilishi wa walimu wenye ulemavu, mwakilishi wa walimu vijana, mwakilishi wa walimu wanawake, mjumbe wa kamati ya utendaji ya Tucta, wadhamini watatu, na vitengo mbalimbali vya chama.

Majina ya wagombea

Wanaogombea nafasi ya Rais mbali na Leah Ulaya anayetetea kiti chake pia yupo makamu wake wa sasa, Ikomba Suleiman huku wengine wakiwa ni Barua Mwalimu, Chakupewa John, Ikomba Suleiman, Julius Shangweli, Kasimba Robert, Kondowe Emmanuel, Mahenga Hamisi, Malinga Ally, Mlobi Stephen, Mudui Charles.

Wengine ni Munyimbegu Rajabu, Mussa Ismaili, Mutungi Ngamera, Ndomba James, Ndonyalo Godhard, Nyatega Rose,  Twambo Tumaini.

Wanaowania nafasi ya Makamu wa Rais ni Bakuza Dennis, Banda Juma, Gabriel Petro, Kajuni Nelusigwe, Kanji Hassan, Kingwala Tatu, Lipukila Sabina, Mahewa Lameck, Malingishi Seleman, Mohamed Mswadiku, Mshana Aziza, Mtembo Bakari, Mtundua Hamisi, Mwabungulu Shaban, Pandisha Robert, Sane Lazaro, Tarimo James, Tung’ombe John, Yahewa Joel.

Sababu kujitokeza wengi

Kuwapo kwa idadi kubwa ya wagombea kumeelezwa na aliyekuwa Rais wa CWT, Gratian Mukoba kwamba ni ishara ya mvuto wa chama kwa kuwa hakuna mtu atakayekubali kuongoza kitu kisichokuwa na maana.

“Japokuwa na zamani walikuwa wanajitokeza kwa wingi hadi 70, lakini ilikuwa katika nafasi za chini. Lakini sasa nafurahi kuona watu wanajiamini na kuzitaka nafasi za juu, jambo ambalo halikuwapo awali, hii inaonyesha namna gani wanajiamini na kuona uongozi hauhitaji nguvu kubwa,” amesema Mukoba.

Amesema ni vyema kwa kiongozi atakayechaguliwa sasa apiganie masilahi ya walimu hususani mshahara, uku akitolea mfano wa mtu anayelipwa Sh1 milioni kwa mwezi kuwa ni ndogo na haikidhi mahitaji kwa maisha ya sasa.

“Mshahara mmoja wa mwalimu ni sawa na posho za vikao vitatu vya mbunge. Mbunge huyu anayelipwa fedha nyingi ndiye anayeenda kukutana na mwalimu katika bucha moja, duka moja, wanaumia sana walimu ni vyema hili alisimamie,” amesema Mukoba.

Katika eneo lingine ametaka watakaochaguliwa kupigania mazingira mazuri ya kazi kwa walimu, ikiwemo nyumba karibu na shule wanazofanyia kazi kwa kuwa maeneo mengi hazipo.

“Huenda wanaoingia sasa hivi wakahisi kukosekana kwa nyumba ni jambo la kawaida kwa sababu hawakuzikuta, lakini ni vyema wahakikishe zinakuwapo ili walimu waweze kufanya kazi kikamilifu,” amesema Mukoba.

Kuhusu nyumba za walimu alizozungumzia Mukoba, Takwimu Msingi (BEST) zinazotolewa na ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) mwaka 2020, zilionyesha kuwapo kwa uhaba wa nyumba za walimu kwa shule za msingi nchini ni asilimia 81.3.

Takwimu hizo zinaonyesha kuna nyumba 46,904 kati ya 251,052 zinazohitajika, ikimaanisha kuwa nyumba moja inategemewa na walimu sita hadi saba, kutokana na idadi ya walimu 194,736 waliokuwepo nchini mwaka huo.

Mikoa yote ina upungufu wa nyumba wa zaidi ya asilimia 50, huku halmashauri 179 kati ya 185 zikionyesha zina upungufu wa asilimia 50 au zaidi.

Dar es Salaam inaongoza kwa upungufu wa asilimia 91, ikifuatiwa na mikoa ya Shinyanga asilimia 87, Kilimanjaro 87, Tabora 87, Tanga 86 na Mwanza 86.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *