Hayo yamesemwa jijini Nairobi nchini Kenya kwenye kongamano linalowaleta pamoja mawaziri kutoka barani Afrika, wataalamu wa mifugo, wadau wa maendeleo na wawakilishi wa sekta binafsi.
Mwakilishi wa kanda ya Afrika, wa Shirika la Chakula na Kilimo-FAO, Abebe Haile-Gabriel amewaambia wajumbe katika mkutano huo, kuwa ngamia wana mchango muhimu katika kukuza maendeleo endelevu yanayokabiliana na vita dhidi ya njaa, kuondoa umaskini wa kupindukia na pia kuwawezesha wanawake kiuchumi.
“Pembe ya Afrika – ikiwemo nchi za Somalia, Ethiopia, Sudan, na mwenyeji wetu Kenya, ni kitovu cha ngamia ulimwenguni. Katika kipindi hiki ambapo tunakumbana na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi, ngamia ana uwezo wa kustahimili ukame,” alisema Haile-Gabriel.
Njaa kutokana na ukame mbaya
Itakumbukwa kuwa mamilioni ya watu katika eneo la pembe ya Afrika wamekabiliwa na baa la njaa katika miaka ya karibuni kutokana na hali mbaya ya ukame uliokumba nchi za eneo hilo tokea mwaka wa 2020 hadi 2023 na kuangamiza idadi kubwa ya mifugo, hasa ng’ombe, kondoo, na mbuzi.
Raison Seketeti ni mfugaji wa kuhamahama, wa jamii ya Wasamburu toka Kaunti ya Laikipia nchini Kenya.
“Tunatembea masafa marefu kutafuta maji ya kunywa na maji safi kwa wanyama wetu. Wanyama wetu wamekonda, wamedhoofika [kiafya]. Wameshusha hata kilo. Ukipeleka sokoni kuuza hakuna kitu utapata. Sasa hata watoto wetu hawaendi shule tena kwa sababu hatuna kitu tunategemea kabisa. Na ujumbe wangu kwa hao wataalamu [ni kwamba] kama inawezekana mtenge pesa za kutosha kunua mifugo yetu wakati wa kiangazi,” alisema Seketeti.
Katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huo, Moses Vilakati, Kamishna wa Tume ya Umoja wa Afrika anayehusika na Kilimo na Maendeleo ya Vijijini amesema ripoti ya hivi karibuni kuhusu chakula na lishe bora inatia shaka, kutokana na idadi kubwa ya watoto barani Afrika walio na viwango vya juu vya utapia mlo licha ya kwamba bara hilo lina utajiri mkubwa wa mifugo.
Mawaziri wa mataifa mbalimbali wahudhuria
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Huyam Salih, mkurugenzi wa mpango wa kuinua jamii za wafugaji, Vilakati, aliye raia wa Eswatini, amesema.
“Kuna nchi kadhaa barani Afrika zinazotumia kiwango cha chini sana cha madini ya proteini yanayopatikana katika maziwa au nyama ya mifugo – yaani kilo tatu hadi tano tu ya proteini, ilhali utafiti unaonesha utumiaji wa mara kwa mara wa aina hiyo ya proteini una manufaa kutokana na virutubisho vingi vyenye kinga ya magonjwa mbalimbali mwilini,” alisema Salih.
Miongoni mwa wanaohudhuria kongamano hilo ni mawaziri kutoka nchi mbalimbali, viongozi wa serikali, wanasayansi, na wataalamu wa mifugo kutoka mashirika ya umma na sekta ya kibinafsi.
Mkutano huo wa siku tatu, utalenga zaidi kujadili mifumo ya chakula na ufugaji barani Afrika, na pia ufugaji wa ngamia ambao wanastahimili mazingira magumu ya maeneo kame, ili kuhakikisha utoshelevu wa chakula kwa wote.