Maelfu ya waandamanaji wanaotaka kuachiliwa huru waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Imran Khan anayetumikia kifungo jela wamekaidi vizuizi vya barabarani vilivyowekwa na Polisi na gesi ya kutoa machozi waliyomiminiwa na askari hao katika azma yao ya kuingia katika mji mkuu Islamabad.
Mapema leo, waandamanaji walikabiliana na polisi waliowafyatulia gesi ya kutoa machozi na risasi za mpira kwenye lango la barabara ya magharibi kuelekea Islamabad.
Tovuti ya habari ya gazeti la The Express Tribune imeripoti kuwa baada ya kukishinda kizuizi cha polisi, misafara hiyo ya waandamanaji imeendelea na safari yao, huku magari yaliyojaza masafa ya umbali wa kilomita mbili yakitangulia mbele kuongoza maandamano hayo.
Khan alizuiliwa kugombea katika uchaguzi wa Februari ambao ulikumbwa na madai mengi ya wizi wa kura, uliowekwa kando na kesi kadhaa za kisheria ambazo anadai zilipitishwa ili kuzuia kurejea kwake madarakani na katika ulingo wa siasa.

Mchezaji huyo wa zamani wa kriketi aliyegeuka kuwa mwanasiasa amefungwa jela tangu Agosti 2023, akikabiliwa na mlolongo wa kesi na mashtaka ya kisheria kuanzia ya ndoa haramu hadi ufisadi na kuchochea ghasia.
Chama chake cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) kimekaidi ukandamizaji wa serikali kwa kufanya maandamano ya mara kwa mara yanayolenga kuhodhi maeneo ya umma huko Islamabad na katika miji mingine mikubwa.
Mji mkuu huo wa Pakistan umewekewa vizuizi tangu mwishoni mwa Jumamosi, na mawasiliano ya intaneti yamekatwa huku zaidi ya polisi 20,000 wakifurika mitaani, wengi wakiwa wamebeba marungu na ngao za kutuliza ghasia.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Dawn, maandamano hayo yalipangwa kufanyika Novemba 24, lakini misafara hiyo ilipumua jana usiku baada ya viongozi wa PTI kusema hawakuwa na “haraka” ya kufika mji mkuu Islamabad kwa maandamano yao waliyoyaita ya “kufa na kupona”…/