Zaidi ya wafanyakazi 100 wa Shirika la Utangazaji la Serikali ya Uingereza (BBC) wamelishutumu shirika hilo kwa kusambaza habari zinazoupendelea utawala wa Israel wakati wa kuripoti vita vya zaidi ya mwaka mmoja vya mauaji ya kimbari vya utawala huo dhidi ya Wapalestina huko Gaza.
Katika barua iliyotumwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa BBC Tim Davie, iliyotiwa saini na zaidi ya wafanyakazi 230 wa tasnia ya habari, wakiwemo wafanyakazi 101 wa BBC ambao majina yao hayakutajwa, BBC imetakiwa “kujitolea tena kutetea haki, usahihi na kutopendelea upande wowote” wakati wa kuripoti mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na Isreal huko Gaza.
Gazeti la The Independent ambalo limeiona barua hiyo limeandika kuwa: “Barua hiyo inalaani shirika hilo kwa kupuuza viwango vyake vya uhariri na kutozingatia “uandishi wa habari wa haki na sahihi mara kwa mara katika uandishi wake kuhusu Gaza.”
Barua hiyo pia imetiwa saini na mwanasiasa wa Uingereza Sayeeda Warsi na mwigizaji Juliet Stevenson na inatoa wito kwa BBC kuripoti “bila woga au upendeleo.”
Warsi alijiuzulu kutoka chama cha upinzani cha Wahafidhina au Conservative mnamo Septemba, akisema kilikuwa kimechukua misimamo mikali ya mrengo wa kulia.
Wengine waliotia saini barua hiyo ni pamoja na mwanahistoria William Dalrymple, Dk. Catherine Happer, mhadhiri mkuu wa sosholojia na mkurugenzi wa vyombo vya habari katika Chuo Kikuu cha Glasgow, Rizwana Hamid, mkurugenzi katika Kituo cha Ufuatiliaji wa Vyombo vya Habari, na mtangazaji John Nicolson.
Barua hiyo inaitaka BBC kuwajibika katika uhariri. Wameitaka BBC “kuwafahamisha wasikilizaji na watazamaji kwamba Israeli haiwapi waandishi wa habari wa kimataifa fursa ya kuingia Gaza; na kuweka wazi wakati hakuna ushahidi wa kutosha kuunga mkono madai ya Israeli; kuweka wazi katika vichwa vya habari kwamba Isreal ndie mtenda jinai na hasa kufafanua muktadha wa kihistoria uliotangulia Oktoba 2023; na kuwapa changamoto vikali wawakilishi wa utawala na jeshi la Israeli katika mahojiano yote.”

Mfanyikazi wa sasa wa BBC ambaye ametia saini barua hiyo ameliambia gazeti la The Independent kwamba baadhi ya wafanyakazi wenzao wameacha kazi kutokana na shirika hilo kupendelea Israel wakati wa kuripoti matukio ya Gaza.
Si mara ya kwanza kwa BBC kukosolewa kwa kupendelea Israel wakati wa vita vya Gaza.
Mnamo Septemba, BBC ilishutumiwa kwa kuzuia kuzinduliwa kampeni ya kitaifa ya televisheni nchini Uingereza kwa ajili ya kuchangisha fedha za misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.