
Kwa miaka ya hivi karibuni, benki zimeonyesha uthabiti mkubwa kwa kupata faida inayotokana na mikakati madhubuti ya kifedha, uboreshaji wa huduma na upanuzi wa mikopo kwa wateja.
Faida hizi hazinufaishi tu taasisi za kifedha, bali zina mchango mkubwa katika uchumi kwa kusaidia biashara ndogo na za kati.
Kwa mfano, mwaka 2024, Benki ya CRDB ilipata faida ya Sh550.8 bilioni, huku NMB ikirekodi faida ya Sh644bilioni.
Ukuaji huu unatokana na mapato ya riba kutoka kwa mikopo, ada za huduma na biashara ya fedha za kigeni.
Faida hii haiishii kwa benki pekee, bali inawezesha sekta mbalimbali kupata mitaji kwa ajili ya kupanua shughuli zao za kiuchumi.
Benki zinazopata faida kubwa zina nafasi kubwa ya kufadhili uchumi kwa kupanua huduma zao za kifedha, kupunguza gharama za mikopo na kuvutia uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Wajasiriamali wadogo ni sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania, wakichangia ajira na uzalishaji wa bidhaa na huduma.
Kupitia faida wanayopata, benki zinaweza kusaidia kundi hili kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuwawezesha kukuza biashara zao.
Wajasiriamali wanaweza kutumia mikopo hiyo kuongeza mtaji kwa kununua bidhaa kwa wingi, kuboresha vifaa vyao vya uzalishaji na kupanua huduma zao.
Kwa mfano, mikopo ya kilimo inaweza kuwasaidia wakulima wadogo kununua pembejeo bora, wakati mikopo ya biashara inaweza kusaidia wafanyabiashara kuongeza bidhaa kwenye maduka au viwanda vidogovidogo.
Benki zinaweza kusaidia wajasiriamali kwa kuwekeza katika mifumo ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha.
Benki zinaweza kuboresha mifumo ya malipo ili kurahisisha upokeaji wa malipo kwa njia salama na ya haraka, hivyo kuongeza ufanisi katika biashara.
Uwekezaji wa benki katika teknolojia unarahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wajasiriamali wengi zaidi, hata walioko maeneo ya vijijini.
Namna nyingine ambayo benki zinaweza kuchangia ni kutoa ruzuku kwenye elimu ya kifedha.
Elimu hii ni nyenzo muhimu kwa wajasiriamali ili waweze kusimamia biashara zao kwa ufanisi.
Benki zinaweza kutumia sehemu ya faida zao kuendesha programu za mafunzo kwa wafanyabiashara wadogo kuhusu mbinu bora za usimamizi wa fedha.
Mafunzo haya yanaweza kuwasaidia kujifunza namna ya kutenga fedha za biashara na matumizi binafsi, kufahamu umuhimu wa mikopo na kujua jinsi ya kutumia mikopo kwa manufaa ya muda mrefu.
Pia, benki zinaweza kuwapa wajasiriamali elimu kuhusu njia bora za kuweka akiba, kupanga bajeti na kudhibiti madeni, ili waweze kuwa na uthabiti wa kifedha.
Benki zinaweza kuboresha ufanisi wa ndani na kupunguza gharama zisizo za lazima kwa wateja na kuhakikisha mfano, mabenki yanaweza kupunguza hitaji la kuongeza ada na tozo kwa wateja.
Hii inaweza kujumuisha matumizi ya teknolojia za kisasa na kuboresha michakato ya ndani ili kuongeza ufanisi.
Kwa jumla, ni vizuri kwa benki kupata faida kuliko kurekodi hasara.
Faida za benki zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Tanzania na kusaidia maendeleo ya biashara ndogo na za kati, hivyo benki ziangalie namna faida hizi zinavyoweza kuboresha mazingira ya wateja wake.
Hatua thabiti zikichukuliwa zitasaidia kuongeza ajira, kukuza uchumi wa ndani na kuimarisha uthabiti wa kifedha kwa wananchi wengi zaidi.