Wafanyabiashara kutoka Italia, Zipa wajadli fursa za uwekezaji

Unguja. Wafanyabiashara na wawekezaji zaidi ya 33 kutoka Italia wamekutana na wenzao kutoka Zanzibar na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa) kujadili maeneo ya uwekezaji ikiwemo nishati, kilimo na michezo ili kuibua fursa mpya na kuwekeza.

Akizungumza katika mkutano huo wa kibiashara (B2B), Februari 14, 2025, Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi na Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff amesema ushirikiano wa pamoja baina ya wafanyabiashara wa nchi hizo na Zanzibar ni wa muda mrefu lakini kwa sasa wapo kwa lengo la kuibua fursa na nafasi mpya za uwekezaji.

Amesema mkutano huo umelenga kukuza ushirikiano baina ya taasisi binafsi na kusimamia biashara na uwekezaji kisiwani.

Amesema wafanyabiashara kutoka nchi hiyo wapo tayari kuwekeza zaidi katika biashara za moja kwa moja, kuhimiza wawekezaji na kusimamia ushirikiano baina yao na taasisi binafsi katika ukanda huu.

Shariff amesema uwekezaji umekuwa kwa kasi na hayo yote yanatokana na mazingira mazuri yaliyowekwa ya kuwavutia wawekezaji na ndiyo maana wafanyabiashara kutoka nchini hiyo wamevutika kuja kutafuta fursa hizo za kibiashara.

“Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji ikiwemo miundombinu, majengo ya biashara na kutengeneza sera na sheria rafiki kwao, ili kuwavutia wawekezaji,” amesema Shariff.

Amesema sera na sheria zilizopo kwa sasa zimebeba vivutio vingi vya uwekezaji ambavyo vitaimarisha biashara kwani sheria hiyo imefafanua vivutio vilivyopo kwa kila sekta, lengo likiwa ni kuwavutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali.

“Serikali imejipanga kufafanua vivutio vyote vilivyopo katika sekta zote kwa lengo la kuwavuta wawekezaji kuwekeza,” amesema Shariff.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Zipa, Saleh Saad Mohammed amesema wafanyabiashara hao waliokutana hapo wanatoka katika jumuiya ya wafanyabiashara nchini Italia wapo kuangalia fursa za biashara kisiwani hapa.

Amesema uwekezaji ambao umeingizwa na wafanyabiashara kutoka nchi hiyo una thamani ya Dola za kimarekani Sh1.1 bilioni sawa na Sh 2.6 trilioni ambao umetengeneza ajira 6,397.

“Ujio wa wafanyabiashara hao ni mwendelezo wa ushirikiano uliowekwa na viongozi katika kuhakikisha tunalinda diplomasia ya uchumi baina ya nchi hizi mbili,” amesema Saleh.

Balozi wa Itali nchini Tanzania, Giuseppe Coppola amesema anakuona nchi yao imekuwa sehemu ya kufanya uwekezaji kisiwani hapa kwani wanatambua uchumi wao umekuwa na kuwavutia wawekezaji wengi.

Hivyo, wafanyabiashara kutoka nchi hiyo wapo tayari kukaa pamoja na kujadili fursa zilizopo kwa lengo la kuwekeza.

Mjumbe kutoka Jumuiya ya wafanyabiashara Zanzibar, Slim Abdalla amesema uwepo wa mikutano hiyo inakuza ushirikiano na ni neema kwao kwani biashara kubwa inayotoka kisiwani hapa inafanyika Itali.