Wafanyabiashara 35 wa Saudi Arabia kuwekeza Zanzibar

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar bado ina fursa nyingi za uwekezaji, hivyo amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Saudi Arabia kuja kuweleza nchini.

Dk Mwinyi ameeleza hayo leo Jumatano, Februari 12, 2025 wakati akizungumzia na timu ya wawekezaji na wafanyabiashara wa nchi hiyo Ikulu Zanzibar.

Amesema kipaumbele cha Serikali ni maeneo makuu mawili ikiwamo sekta ya utalii inayoingiza asilimia 30 ya pato la Zanzibar na sekta ya uchumi wa buluu.

Hata hivyo, maeneo mengine ni kilimo, biashara na mafuta na gesi.

Hivyo aliwahakikishia wawekezaji na wafanyabiashara kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao ili kuona uchumi wa Zanzibar unaendelea kukua zaidi.

“Bado kuna nafasi kubwa ya kuwekeza hususani katika utalii, kilimo na mafuta na gesi,” amesema.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Sharif Ali Sharif amesema ujumbe huo umetokana na kongamano la biashara na uwekezaji lililofanyika mwaka 2024 jijini Riyadh, Saudi Arabia, ambalo liliwashirikisha watendaji wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanzania.

Amesema ujumbe huo ni kuanza ushirikiano wa uwekezaji na wafanyabiashara 35 kuona jinsi gani wanavyoweza kushirikiana katika maendeleo ya uchumi wa nchi mbili na wengi wao wana nia na wamevutiwa na vivutuo na fursa zilizopo Zanzibar.

“Tumepokea miongozo ya Rais Mwinyi aliyowapatia kuhakikisha wawekezaji hao wanapewa kila aina ya msaada kwa yale wanayotarajia ili kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa zaidi.”

Waziri Sharif akiyataja maeneo ambayo wameonesha nia ya kuwekeza ni uchumi wa buluu, utalii, nishati, miundombinu na maendeleo ya kilimo.

Kwa upande wa mafuta na gesi Waziri Sharif amesema wawekezaji hao wapo tayari kuja kuwekeza katika eneo biashara.

Rais wa Shirikisho la Jumuiya za Wafanyabiashara Saudia Rabia, Hassan Alhuwayz amesema lengo ni kuja kufungua ushirikiano mkubwa na Zanzibar kwa kuvutiwa na maendeleo yaliyofikiwa lakini pia mazingira kwa kuwa, wamegundua Zanzibar ina fursa wanazoweza kushirikiana kuwekeza na kufanya biashara.

Amesema wamevutiwa na amani na utulivu iliyopo Zanzibar na jinsi Wazanzibari walivyowakarimu na kuahidi kurudi tena kwa ajili ya kutalii lakini pia kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika maeneo muhimu ya uwekezaji.

Wakati huohuo, Dk Mwinyi ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushauri kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya Saudi African Investment and Development Company (SAIDC).

Mkataba mwengine ni hati ya ushirikiano kati ya Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyabiashara la Saudi Arabia, kwa lengo la kuimarisha uwekezaji wa kimkakati na kukuza uchumi wa Zanzibar na barua ya uwajibikaji.