Waendesha bodaboda wakumbushwa sheria ya usalama barabarani, kuepuka ajali

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na ongezeko la bodaboda nchini, madereva wa vyombo hivyo wametakiwa kufuata sheria za usalama barabarani pindi wanapoziendesha kama wanavyoshauriwa na wataalamu ili zidumu kwa muda mrefu na kuepuka ajali.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Usafiri wa  Ardhini (Latra), mwaka2023/24, ilitoa leseni 46,146 (D1) za pikipiki ikiwa ni ongezeko kutoka leseni 31,937 zilizotolewa mwaka wa fedha 2022/23.

Akizungumza leo Alhamisi Machi 6, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati akiipongeza Kampuni ya Alternative Solution Limited inayosambaza pikipiki zenye ubora, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema, “tunao wataalamu hapa leo, naomba tuwasikilize ili matumizi yawe bora pamoja na mambo mengine tupunguze ajali.”  

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaa Albert Chalamila, wakati wa uzinduzi wa pikipiki aina ya Daima na Everlast,  katika viwanja vya TCC Club Chang’ombe, Mapunda amesema, “inapendeza kuona sisi Watanzania wenyewe tukitafuta suluhisho ili kuleta unafuu katika sekta hii ya usafirishaji, kwani pikipiki zinatumika kila mahali nchini na zinarahisisha usafiri wa abiria na mizigo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.”

Mapunda ametoa wito kwa watumiaji wa pikipiki hasa madereva wa bodaboda kufuata sheria za barabarani na kuzingatia matumizi sahihi ya pikipiki.

Pia, ameyataka mashirika mbalimbali ya kifedha yaingie makubaliano na kampuni hiyo ili kuhakikisha waendesha bodaboda wanajengewa uwezo wa kumiliki pikipiki zao wenyewe kwa utaratibu mzuri usiowaumiza.

Amesema tayari Jiji la Dar es Salaam limeanza kufanya kazi saa 24 na moja ya usafiri unaotegemewa na watu wengi ni pikipiki, “uzinduzi huu umekuja muda mwafaka wakati bidhaa hii inahitajika.”

Mkurugenzi wa Kampuni ya Alternative Solution Limited, Ruge Chacha amesema kampuni hiyo ilifanya utafiti wa kina ili kufahamu mahitaji ya Watanzania hususani watumiaji pikipiki kujua changamoto wanazopitia kabla ya kuziagiza.

Chacha amesema pikipiki za Daima na Everlast zina faida nyingi zaidi ikilinganishwa na pikipiki nyingine ikiwamo kuwa na nafasi kubwa ya kukalia dereva, abiria na pa kubebea mizigo.

“Kuna sehemu ya kuhifadhi na kuchajia simu, sehemu ya kuwekea chupa ya maji upande wa kulia na taa imara inayoona vizuri hata wakati wa mvua na giza,” amesema.

Chacha amebainisha kuwa, pikipiki hizo zina matairi imara yanayowezesha kupakia abiria na mzigo mzito bila wasiwasi kwani, kuna sehemu maalumu ya mizigo ambayo pikipiki nyingine hazina.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau wa sekta ya usafirishaji hususan pikipiki na baadhi walipata fursa ya kujaribisha na kuuliza maswali kuhusu pikipiki hizo mpya.

Mbunge wa Temeke, Dorothy Kilave ameahidi kuendelea kushirikiana na waendesha bodaboda wote kwa kuzingatia umuhimu wao katika jamii.

“Zingatieni sheria za barabarani na mnunue pikipiki za Daima na Everlast zitawasaidia,” amesema Kilave.