
Dar es Salaam. Wadau wa siasa nchini wamekuwa na mtazamo tofauti kuhusu hatua ya Chadema kutosaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi 2025, na kuwapo na sintofahamu baina yao na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).
Wakizungumza leo Jumatano Aprili 16, 2025 wakati akichangia mjadala wa Mwananchi X Space wenye mada isemayo: Kanuni za maadili ya uchaguzi 2025 na mustakabali wa siasa za Chadema, ulioandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL).
Wakili Sweetbert Nkuba ameshauri busara na hekima zitumike baina ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ili wafikie mwafaka wa namna watakavyomaliza sintofahamu iliyopo sasa.
“Wakati mwingine sheria zinakuwa na upungufu au kila mtu anatafsiri kulingana na inavyomnufaisha, ndiyo maana mtu anaweza kushinda kesi kwenye Mahakama ya mwanzo na ushindi wake ukatenguliwa Mahakama ya Wilaya akaenda Mahakama Kuu akashinda akaenda Mahakama ya Rufaa ushindi wake ukatenguliwa,”amesema Wakili Nkuba.
Amesema kusainiwa kwa kanuni za maadili za uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni takwa la kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, kinachovitaka vyama vya siasa, Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kusaini kanuni hizo.
Aprili 12, 2025 Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), Ramadhan Kailima alisema Chadema hakitashiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba na chaguzi ndogo zitakazofuata kwa muda wa miaka mitano baada ya chama hicho, kususia kusaini kanuni, hivyo kukosa sifa ya kushiriki mchakato huo.
Akizungumza katika mjadala huo, mwanahabari mkongwe nchini, Absalom Kibanda amesema angekuwa kiongozi wa Chadema, asingefanya makosa kwenye mchakato wa kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi Mkuu zilizotolewa na INEC.
Amesema kwa kusaini tu, chama kingepata fursa ya kushiriki uchaguzi huo na wangeendelea kushikilia msimamo wa kampeni ya No reforms, no election.
Amesema Chadema kabla ya kufikia uamuzi wa kususia, wangerejea kilichotokea mwaka 2013/14 kwenye Bunge la Katiba.
Kibanda ambaye ni mwandishi aliyebobea kwenye uandishi wa habari na makala za siasa amesema Chadema kilisusia kikitarajia baadhi ya mambo yangefanyika lakini haikuwa hivyo.
Naye Mwandishi mwandamizi wa habari za siasa wa Mwananchi, Peter Elias amesema Chadema kisiposhiriki uchaguzi huo huenda kikapoteza nguvu ya ushawishi wake kwa umma kilioujenga kwa muda mrefu.
Amesema uhai wa chama chochote cha siasa ni pamoja na kushiriki chaguzi zinazofanyika na kutimiza malengo ya kushika dola, lakini ukiwa nje ya mchezo huwezi kupata ushawishi huo.
“Fursa pekee ilivyonavyo vyama vya siasa ni kujijenga kupitia uchaguzi na vikishinda vikapata viti vinakuwa na sauti bungeni katika kuwakilisha wananchi,”amesema Peter.
Katika maelezo yake amekishauri Chadema kuona haja ya kufanya mazungumzo ya maridhiano kama ilivyoshauriwa na baadhi ya viongozi wastaafu kwa kuwa ni jambo linalozungumzika katika kutafuta mustakabali wao.
Naye mwanahabari na mdau wa siasa, Elias Msuya amesema haoni madhara makubwa yatakayojitokeza endapo chama hicho hakitashiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Kwa mujibu wa Msuya, ukisikiliza kauli za baadhi ya viongozi wa chama hicho, zinaashiria kama hawataki kushiriki uchaguzi huo na badala yake wamejikita kunadi ajenda ya No reforms, no election ili kushinikiza Serikali kufanya mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi.
“Chadema kilikaa bila wabunge, lakini kiliendelea kujiimarisha, sioni madhara makubwa endapo Chadema kisiposhiriki uchaguzi, sioni madhara kwa sababu hata wakishiriki hawatapata kitu,”amesema Msuya.
Kutokana na hilo, Msuya amekishauri Chadema kuendelea na kampeni yake ya No reforms, No election akisema ipo siku mabadiliko yatapatikana, hata kama sio katika uchaguzi wa mwaka 2025.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa akizungumzia ni kwa nini wameivaa INEC, amedai kuwa imesema uongo kuhusu kanuni za uchaguzi wa 2025.
“Tulilazimika kulizungumza jambo hili kwa sababu tulijiridhisha baada ya kukaa na kupitia maeneo kadhaa tukabini na kuona alichokisema Mkurugenzi wa Uchaguzi ni uongo, na afanya hivyo akiwa anajua anasema uongo ili atengeneze mjadala,” amesema Golugwa.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele alisema kilichozungumzwa na tume hiyo ni tafsiri yao, huku akisema kama Chadema wanatafsiri tofauti basi mtafsiri wa mwisho wa mambo hayo ni Mahakama.
“Mahakama ni mtafsiri wa mwisho inaweza kusema kipi sahihi, ni suala la kutafsiri tu Katiba imesema hivi na sheria zinasema hivi na Kanuni zinasema hivi kwa hiyo msimamo ni upi. Tume huru ya Uchaguzi tulitoa tafsiri yetu maana yake wewe usipo saini hutashiriki kwenye uchaguzi,”alisema jaji huyo.
Kulingana na Jaji Mwambegele taasisi hiyo haitaki kubishana na Chadema kwenye mitandao ya kijamii huku akieleza kwanza wameshatoa msimamo hawana nia ya kushiriki uchaguzi.
“Sasa mbona wanataka tuanze kubishana kwenye tafsiri, ni sawa uko na jirani yako unasema utanunua mbuzi nitakuwa na mfunga na kumlishia sehemu hii halafu mnaanza kubishana tena na jirani huwezi kulishia hapa hii si sehemu yako na kuanza kugombana wakati mbuzi mwenyewe hajanunuliwa,” alisema.
Mwambegele alisema amekuwa akisoma kwenye mitandano ya kijamii Chadema wakidai hawatashiriki uchaguzi huo na hawana mpango wa kusaini kanuni.
Lakini Golugwa amesema msimamo wa chama hicho kutosaini kanuni za uchaguzi Mkuu 2025, wanajiona wako sawa huku akikisisitiza hawatakimbilia kuzisaini zaidi ya kufichua yasiyofaa.
“Tunaona tunaenda sawa kabisa na watu wanazungumza operesheni yetu ya ‘No reforms, no election’ hivyo mkakati huu tunaenda nao sawa kabisa,” amesema.
“Hili la kanuni hatutafuti kuridhiana hapa, hapa tunatafuta mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, hatutakimbilia kusaini kanuni isipokuwa tutaendelea kuyasema yanayotakiwa kufanyiwa mabadiliko,” amesema Golugwa.
Amesema kanuni hizo zinatumika kama fimbo ya kuvichapia vyama vya upinzani.