Wadau watoa neno vipaumbele vya elimu 2025/26

Wadau watoa neno vipaumbele vya elimu 2025/26

Mwanza. Wakati Bunge lilipitisha bajeti ya elimu kwa mwaka 2025/26, wachambuzi na wadau wa elimu wameelezea hisia zao kuhusu vipaumbele vilivyowekwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Bajeti hiyo ya Sh2.4  iliwasilishwa bungeni Mei 12, 2025 na Waziri Elimu, Profesa Adolf Mkenda kisha, Bunge kuipitisha, ikiwa imeongezeka kwa asilimia 23.8 sawa na Sh0.469 trilioni ikilinganishwa na ya mwaka 2024/25 iliyokuwa Sh1.97 trilioni ikiwa na vipaumbele vitano.

Vipaumbele hivyo ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa sera na mitalaa, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji wa elimu na mafunzo, kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo vya ufundi na mafunzoya ufundi stadi.

Pia, kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu, kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na kuimarisha uwezo wa nchi katika utafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchangia upatikanaji wa maendeleo endelevu.

Maoni ya wadau

Wakizungumza na Mwananchi, wadau hao wameeleza kuwa bajeti hiyo haitoi majibu ya moja kwa moja kwa changamoto zilizopo kwenye mfumo wa elimu nchini, licha ya kuonyesha mwelekeo mzuri wa kisera.

Mchambuzi na mdau wa elimu,  Muhanyi Nkoronko anasema vipaumbele hivyo vinaweza kuleta mabadiliko chanya kwa asilimia fulani, lakini utekelezaji wake utakutana na changamoto kubwa.

Akizungumza kuhusu hali halisi katika shule, Nkoronko anasema bado kuna uhaba mkubwa wa majengo, walimu, na vitendea kazi katika shule za msingi na sekondari hasa vijijini.

“Vipaumbele hivyo vinaonekana kuwa na manufaa, lakini kuna mambo muhimu ambayo bado hayatekelezwi ipasavyo. Hii inajumuisha uhaba wa majengo ya shule, waalimu, na vifaa vya kufundishia,” anasema Nkoronko.

Anaongeza kuwa ingawa fungu linalopelekwa kwenye sekta ya elimu ni halisia, bado kuna hatua zinazohitaji kufikiwa ili vipaumbele hivyo vifanikiwe.

Anaeleza kuwa vipaumbele vitano vilivyowekwa vinahitaji kujisimamia vyenyewe, ili viweze kutekelezwa kwa ufanisi, huku akisisitiza kuwa kutekelezwa kwa vitendo ni muhimu kwa maendeleo ya elimu nchini.

Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Mtakatifu  Agustino (Saut) kilichopo mkoani Mwanza, Mariasalome Agustino anasema vipaumbele vya bajeti hiyo havikidhi ubora wa elimu inayotakiwa, kwakuwa mdukumo umeelekezwa  kwa mwanafunzi badala ya vifaa vya kufundishia.

“Sana sana wangezidisha vifaa vya kufundishia, wasijali kwamba hii ni taasisi binafsi ya elimu au ya Serikali. Wangewekeza katika ufundishaji na utafiti kuliko mikopo wanayowapa wanafunzi,”anasema na kuongeza:

“Kama Serikali inaona elimu ni kipaumbele katika hili Taifa wasiangalie tu kwenye vyuo au taasisi za Serikali waje na binafsi hasa kwenye utafiti pamoja na vifaa hasa vya engineering (uhandisi), uwekezaji wake ni mkubwa sana kwahiyo vile vyuo vinavyojikita kwenye sayansi na teknolojia ambavyo ndiko dunia inakoelekea wangewekeza bila kujali ni vya Serikali au binafsi,”

Kwa upande mwingine, anasema elimu inayotolewa ina changamoto kwakuwa imejikita kwenye nadharia badala ya vitendo kuanzia shule za msingi.

“Japo imeboreshwa lakini bado hatujafanikiwa. Kwa mfano walivyoanza  elimu amali..hiyo ni nzuri kwahiyo wale ndiyo wangependelewa na kupewa kila kitu wanachohitaji nafikiri ingekidhi,”anaeleza.

Mdau wa elimu ambaye pia ni mwalimu mstaafu, Catherine Sekwao anasema: “Tatizo kubwa ambalo bado halijafikiwa ni suala la vitendea kazi na walimu wa shule za msingi hasa tunapozungumzia maeneo ya vijijini..walimu hawana nyumba za kukaa, wanatumia gharama kubwa za nauli kukodi usafiri.”

Anaongeza kuwa bajeti hiyo bado hairidhishi kutokana na makubaliano ya hapo awali kushindwa kufikia matarajio ambayo yalikuwa ni kufikia kiwango cha asiimia 27. 

“Wangemfikiria  huyu mwalimu wakampa mazingira mazuri ya  kufundishia..ni motisha kubwa hivyo sijaridhika navyo (vipaumbele)kwa sababu huko nyuma mawaziri walikubaliana kwamba bajeti ya elimu iwe asilimia 20 lakini bado hatujafika huko,”anaongeza.

Msimamizi wa miradi ya elimu kwa wasichana kutoka Shirika la Haki Elimu Wilaya ya Kigoma Vijijini (GCRCI), Esha Mbise, anasema bajeti hiyo bado haijaakisi vipaumbele vilivyotangazwa na wizara.

“Ili tufike ambapo tumedhamiria kufika kama tumedhamiria bajeti ingeongezwa walau hata trilioni tatu ili vifaa vionekane. Japo kwa sasa wizara inaonyesha mwelekeo mzuri katika mageuzi ya kielimu, lakini utafikaje huko wakati wanafunzi bado wanakaa 200 kwenye darasa moja? Kwa bajeti hiyo kompyuta ngapi zitanunuliwa?” anahoji Esha.

Anasema pamoja na nia njema ya mageuzi ya kielimu,  kuna pengo kubwa kati ya matarajio na uwekezaji wa kifedha, hasa katika maeneo ya elimu ya amali na vyuo vya ufundi.

“Japo bajeti bado iko chini, unapozungumzia suala la utafiti unahitaji fedha za kutosha. Elimu ya amali inahitaji fedha za kutosha. Sasa kwa bajeti hiyo mtoto anayejifunza ufundi bomba, mabomba yatanunuliwa ya kutosha au kompyuta kwa kila shule za kutosha?”anahoji.

Naye, Ofisa Elimu wa Wilaya ya Kibondo, Oliver Winfred anasema bajeti hiyo inatoa mwelekeo mzuri wa kisera, lakini utekelezaji wake utategemea sana kama fedha hizo zitatolewa kwa wakati na kusimamiwa ipasavyo.

“Kwa sasa elimu ya awali inaelekeza iwe na walimu waliopata mafunzo ya ujifunzaji na ufundishaji kwa ajili ya watoto wadogo chini ya miaka mitano. Lakini kama kwenye vyuo hakutakuwa na bajeti ya kuwapokea walimu wanaokwenda kupata haya mafunzo, na kama hatutakuwa na miundombinu ya kutosha, bajeti haitakuwa imesaidia,” anasema.

Anashauri kuwa kila shule inapaswa sasa kuwa na darasa la elimu ya awali, walimu wenye mafunzo maalum, vifaa na madarasa yaliyokidhi viwango, jambo linalohitaji bajeti ya kutosha.

Mwalimu wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Binza (Binza VTC), wilaya ya Maswa, Mabula Daniel anasema vipaumbele vya bajeti vinaonyesha dhamira njema ya Serikali, lakini akasisitiza umuhimu wa utekelezaji wenye uwazi na ufanisi.

“Hii ni hatua nzuri kwani inaweka msingi wa kujenga mfumo wa elimu unaoendana na mahitaji ya karne hii. Kuna nia ya kuboresha ubora, kuongeza fursa za upatikanaji, na kuandaa wanafunzi kwa soko la ajira na uchumi wa kisasa kupitia elimu ya amali na ubunifu,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *