Wadau wataka uwekezaji zaidi miradi ya umwagiliaji

Wadau wataka uwekezaji zaidi miradi ya umwagiliaji

Njombe. Wakati Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ikiwasilisha ombi la kuidhinishiwa bajeti ya Sh382.13 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026, wadau wa sekta ya kilimo wameitaka Serikali kuweka kipaumbele katika ujenzi wa miradi ya kimkakati ya umwagiliaji.

Wamesema hatua hiyo itasaidia kukuza kilimo endelevu na cha uhakika, ambacho hakitegemei tena mvua, hasa wakati huu ambapo mabadiliko ya tabianchi yameathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mazao nchini.

Wito huo umetolewa leo, Mei 22, 2025, na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Pembejeo za Kilimo Mkoa wa Njombe, Abusalum Magoma, alipokuwa akizungumza na Mwananchi Digital akiwa mkoani hapa.

Magoma ametoa wito huo ikiwa ni siku moja tangu Wizara ya Kilimo kupitia waziri wake, Hussein Bashe, kuomba bajeti ya Sh1.2 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake katika mwaka wa fedha ujao.

“Kilimo cha kutegemea mvua ni cha kubahatisha. Mkulima ananunua mbegu, anapanda, lakini mvua haiji, anaishia kupata hasara. Tunahitaji mfumo utakaomwezesha mkulima kulima muda wote bila kutegemea mvua,” amesema Magoma.

Aidha, ametoa wito kwa Serikali kuhakikisha bajeti ya Wizara ya Kilimo inaendelea kupewa kipaumbele ili kuanzisha mashamba ya kuzalisha mbegu ndani ya nchi, badala ya kutegemea mbegu na mbolea kutoka nje.

Maoni hayo yameungwa mkono na mkulima kutoka Njombe, Eniadi Fungamila, ambaye aliiomba Serikali kuhakikisha mbegu zinafikishwa kwa wakulima vijijini kwa wakati na kwa bei nafuu.

“Serikali itusaidie kupata masoko ya mazao yetu. Tusiendelee kupata shida kuuza. Pia, mbegu zifike vijijini kwa wakati ili tusichelewe kupanda,” amesema Fungamila.

Kauli hizo zimetolewa wakati huu ambapo Serikali, kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, imeongeza miradi ya umwagiliaji kutoka 13 mwaka 2020/2021 hadi kufikia miradi 780 mwaka 2024/2025, kwa mujibu wa Bashe.

Miradi hiyo inatarajiwa kufikia eneo la umwagiliaji lenye ukubwa wa hekta 543,366.46, na utekelezaji wake unakadiriwa kugharimu Sh1.345 trilioni. Kukamilika kwa miradi hiyo kutapanua eneo la umwagiliaji hadi hekta 1,270,647.06.

Kadhalika, idadi ya Vyama vya Umwagiliaji vilivyosajiliwa imeongezeka kutoka 19 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 912 mwaka 2024/2025. Kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji Na. 4 ya mwaka 2013, vyama hivyo vina jukumu la kuhakikisha uendelevu wa miundombinu ya umwagiliaji.

Waziri Bashe pia ameeleza kuwa Tume ya Umwagiliaji imenunua mitambo 18 ya uchimbaji wa visima, pamoja na magari madogo 58 kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi.

Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Tume ya Umwagiliaji imeomba kuidhinishiwa Sh382.13 bilioni, ambapo Sh308.72 bilioni zimetengwa kwa ajili ya maendeleo, na Sh73.41 bilioni kwa matumizi ya kawaida.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *