
Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya siasa nchini wamependekeza uwepo ukomo wa ubunge na udiwani wa viti maalumu, wakieleza baadhi yao wamehodhi nafasi hizo wakizitumikia kwa hadi miaka 25.
Pia imeelezwa ni muhimu kuwapo utashi wa vyama vya siasa kuwawezesha wanawake kugombea kwenye majimbo, huku mchakato wa kuwapata viongozi hao usitokane na vyama.
Wameeleza hayo leo Jumatano Machi 5, 2025 wakichangia mjadala wa Mwananchi X Space uliojadili mada isemayo: “Ni sahihi kuwa na ukomo ubunge, udiwani viti maalumu” ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).
Februari 28, 2025 hoja ya ukomo wa viti maalumu iliibuka katika maadhimisho ya miaka 15 ya kuanzishwa kwa Umoja wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo) jijini Dar es Salaam sambamba na kuadhimisha miaka 30 baada ya azimio la Beijing kuhusu haki za wanawake.
Katika maadhimisho hayo, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa (UWT), Sophia Simba alisema ifike mahali uwepo ukomo wa viti maalumu ili wengine wakalie nafasi hizo.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kati, Devotha Minja amesema ni sahihi kuweka utaratibu wa ukomo wa ubunge na udiwani wa viti maalumu.
“Dhima ya kuanzisha viti maalumu ilikuwa kusaidia kuongeza uwakilishi wa wanawake kwenye vyombo vya uamuzi kwa maana ya udiwani na ubunge, kujenga uwezo ili wanawake waweze kwenda majimboni,” amesema.
Devotha aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu amesema inapaswa kila baada ya muda fulani mwanamke ajengewe uwezo kwa kufikia malengo yake.
“Tunaamini akipewa miaka mitano ya udiwani au ubunge atakuwa amepata uzoefu na nguvu ya kiuchumi. Kipindi cha miaka mitano kinatosha kabisa,” amesema.
Amesema bahati mbaya viti maalumu vimekuwa kama ajira kwa baadhi ya vyama vya siasa. Tangu kuanzishwa kwake, anasema historia inaonyesha kuna wanaoingia hadi awamu tano.
“Inakuwaje mtu miaka 25 bado anaendelea kupewa fursa? Ameshapata uwezo na uelewa wa kutosha na anajua hali ya kisiasa ndiyo maana kumekuwa na kigugumizi kwa wenzetu kuweka ukomo wa viti maalumu,” amesema.
Devotha aliyewahi kugombea ubunge jimbo la Morogoro Mjini amesema kupewa nafasi mara nyingi kunawanyima wengine fursa ya kwenda kuonyesha uwezo wao.
Gen-Z wapewe nafasi
Mratibu wa Kitaifa wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa (Ulingo), Dk Ave- Maria Semakafu amesema anatamani wanasiasa wanaochipukia ndio wapate ubunge wa viti maalumu ili wazoefu waende majimbo wakashindane.
“Ningetamani kuona Gen-Z (wanasiasa wanaochipukia) waende kwenye viti maalumu, sisi watu wazima wenye uzoefu twendeni moja kwa moja majimbo kupambana ili kuwapa fursa watoto,” amesema.
Amesema: “Natamani sana kwanza hadhi ya viti maalumu ipandishwe ili kweli wanapokwenda pale wanakuwa wabunge. Huwezi kuwa mbunge, halafu huingii jimboni hadi upewe kibali na mbunge mwenye jimbo lake.
“Huyu anayeitwa viti maalumu haruhusiwi kufanya kitu chochote hadi apate kibali cha mwenye jimbo, la sivyo anajipitishapitisha. Jamani hizi siasa zimepitwa na wakati,” amesema.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Lailah Burhan Ngozi amewataka wanawake kuondoa hofu, akieleza hoja ya kuweka ukomo wa viti maalumu vya ubunge na udiwani ikipita itakuwa na tija.
“Niwaombe kwa sababu nimeona baadhi ya wanawake wameanza kuwa na hofu, wasiwe na hofu kwani huu ni mwanzo mzuri, ikipita itaenda kujenga wanawake jasiri,” amesema.
“Kama mjadala wa ukomo utakuwepo tutaujadili na kuutoa nje kwa sababu hatuna haja ya kuwa na hofu, chama chetu bado hakijaanza kulijadili hili kwa sababu halijafika,” amesema.
Amesema mtindo wa wanawake kusubiri viti maalumu na kubebwabebwa hauwezi kuwa na tija na hautawezesha kufikiwa malengo asilimia 50 kwa 50.
“Ifike wakati hata tutakapoamua kupitia vikao basi mimi niwashawishi wanawake wenzangu tukalikubali hilo kwa sababu katika chama chetu tuna Jumuiya ya Umoja wa Vijana inayobeba watoto wa kike katika nafasi mbalimbali za ubunge na uwakilishi kwa upande wa Zanzibar,” amesema.
Utashi wa vyama
Katibu Mkuu wa zamani wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Catherine Ruge amesema vyama vya siasa ni nyenzo muhimu ya kuhakikisha wanawake wanajengewa uwezo wa kuwania majimbo, lakini bado haviamini kama kundi hilo linaweza kusimama.
Ruge aliyewahi kuwa mgombea ubunge wa Serengeti, mkoani Mara, mwaka 2020 amesema mwanamke anaweza kushinda katika kura za maoni, lakini anaambiwa ampishe mwanamume ili yeye apewe viti maalumu.
Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalumu amesema: “Hii maana yake nini, hakuna utashi wa kisiasa, siyo tu kwenye vyama vingine hata kwenye chama changu. Muda mwingine hakuna utashi wa kisiasa wa kweli wa kuwasaidia wanawake.”
“Kwa hiyo hii 50 kwa 50 vyama vya siasa vikiamua inawezekana, lakini kuna ubinafsi wa hali ya juu hasa kwa wanaume wanaotamani wawe wao tu viongozi, lakini pia mtazamo wa jamii kwamba wanawake hawawezi,” amesema.
Mdau wa siasa, John Mbura amesema haoni haja ya kuendelea kuwepo viti maalumu, akidai hakuna kazi wanazofanya bungeni.
Pamoja na hayo, amesema kuna ulazima wa kuwepo ukomo wa miaka mitano ya ubunge na udiwani wa viti maalumu ili kupata sura mpya za uwakilishi katika Bunge na Kata.
“Kuna mazoea fulani yanafanyika, hata bungeni kuna vitu haviendi sawa, kuwepo kwa ukomo ni jambo sahihi kwa sababu tukiwa na aina tofauti ya wabunge na madiwani kunakuwa na utatuzi wa haraka wa changamoto.
“Naona bora tuwe tunapokezana kwa sababu hata wenyewe wakikaa bungeni wanasema vijana tafuteni ajira, sasa tungepokezana hapo kwenye ubunge ili tupeane ajira,” amesema.
Mhariri wa siasa wa Mwananchi, Peter Elias amependekeza kuwepo ukomo wa vipindi viwili vya ubunge, udiwani wa viti maalumu, kama hakuna muda wa kutosha wa kufanya mabadiliko kuhusu suala hilo.
“Nashauri kungekuwa na ukomo wa vipindi viwili au vitatu ili kuwapa nafasi wabunge kupata uzoefu, kisha baadaye waende majimboni, kwa sababu watakuwa na uzoefu wa kushindana katika majimbo,” amesema Elias.
Mwanahabari Elias ameshauri wanawake kupewa nafasi zaidi ndani ya vyama ili kugombea majimbo katika uchaguzi mkuu.
Mchakato usiotokana na vyama
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Kamara Dickson amesema vuguvugu la kuwa na wanawake kwenye vyombo ya uamuzi kupitia nafasi za ubunge na udiwani halikuanzia kwa vyama vya siasa.
“Jambo hili lilianzia kwa wanawake wanaotoka asasi za kiraia walipaza sauti zao baada ya kufanya utafiti na kuona kuna ombwe na wanatakiwa kupigania ili wapate fursa hiyo, ingawa vyama vya siasa vikapoka mchakato na kuanza kupeleka watu wao,” amesema.
Amesema mchakato huo ulipaswa kuwa wa kiraia (usiotokana na vyama)kwa sababu hata uwakilishi wa wanawake wa viti maalumu kupitia vyama, wanakwenda kwa tiketi ya makundi wanayoyawakilisha kama vile kundi la asasi za kiraia na wenye ulemavu.
“Hoja inakuja kama kundi linawakilishwa na mtu anayetoka kwenye chama cha siasa ina maana hilo kundi lenyewe halina uwezo wa kujikusanya kumchagua mtu ambaye ni mwakilishi kuwawakilisha wenzao, inakuwaje hadi wapitie kwenye vyama,” amesema.
Amesema kinachotokea mbunge akienda anabeba ajenda ya chama na kulisahau kundi analoliwakilisha, akieleza hata michango yake haijikiti kulisemea kundi hilo.
“Anabeba ridhaa ya chama badala ya kundi analoliwakilisha,” amesema.