Dar es Salaam. Wadau wa masuala ya ubunifu wamevitaka vyombo vya habari nchini kuongeza kasi ya uandishi wa habari za ubunifu kwa sababu ndiyo dunia inakokwenda.
Ili kufanikisha hilo, wametaka waandishi wa habari kujengewa uwezo wawe wabobezi wa eneo hilo ili kuondoa ombwe lililopo sasa la kuandika vitu wasivyovifahamu kwa undani.
Hayo yamesemwa leo Mei 12, 2025 katika ufunguzi wa wiki ya ubunifu (Innovation week) ambapo wadau wa vyombo vya habari na wabunifu walijadili kwa pamoja jukumu la vyombo hivyo katika kuendeleza ubunifu na ujasiriamali kama ajira kwa vijana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Rosalynn Mndolwa-Mworia akizungumza katika mkutano wa wiki ya ubunifu Tanzania unaofanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Sunday George
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Simplitech, Baraka Cassian amesema bado vyombo vya habari havijui namna bora ya kuandika habari za kampuni changa kwa sababu hawajui vyema ni kitu gani hasa.
“Na hata wanapoandika wanajikuta wanatafuta namna ya kuandika kitu ili kifanye vyema mtandaoni, badala ya kuzifanya zieleweke vyema kwenye jamii,” amesema Cassian.

Mbali na vyombo vya habari amesema hata vijana wenyewe wanapokuja na hizo kampuni changa hawajui kuwa ni kitu kinachoweza kuwakuza kiuchumi.
“Bado vijana wengi wanakosa namna itakayowawezesha kujua bunifu zao zinavyoweza kugeuzwa kuwa biashara na kufaidika nazo. Hivyo vyombo vya habari vinapaswa kuwekeza kwenye kuonyesha kwa upande wa kibiashara ili kuwavutia vijana wengine kuingia huko,” amesema Cassian.
Mwanzilishi wa kampuni ya Waga, Gibson Kawango amesema kuwepo kwa pengo la uelewa kati ya waandishi wa habari imekuwa ikiwafanya washindwe kuuliza maswali magumu yanayoweza kuleta uelewa kwa jamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Rosalynn Mndolwa-Mworia amesema huu ndiyo wakati wa sekta ya habari ya Tanzania kuchukua nafasi yake kikamilifu kama chombo cha mabadiliko ili kuhakikisha habari hizo zinaandikwa kwa wingi.

“Lazima tuache kushindana kwa ajili ya kupata umaarufu na tuanze kushirikiana kwa ajili ya kuleta matokeo chanya, tuwahimize watunga sera kutunga sheria zinazowawezesha wabunifu, tuwatie moyo wafadhili kuwasaidia wajasiriamali wapya na kuhakikisha simulizi kamili kama changamoto, uvumilivu, na mafanikio zinaandikwa,” amesema Mworia.
Kaimu mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), John Rutere amesema mjadala huo ni nafasi ya kufikiri pamoja, kutathmini na kujiuliza nafasi yao katika kuchochea maendeleo ya bunifu.
“Je, vyombo vya habari pamoja na wadau wengine wanawezaje kwenda zaidi ya kuwa watazamaji tu. Je, mnawezaje kusaidia dunia ione ukweli na utajiri wa hadithi za ubunifu wa Tanzania kutoka suluhisho za kijamii hadi miradi mikubwa ya kiteknolojia,” amehoji Rutere huku akieleza kuwa UNDP huweka mkazo katika masuala ya ubunifu ndiyo maana waliamua kuja na mradi wa ‘Funguo’ ili kuwawezesha wabunifu.
Hata hivyo, mbali na kile kilichofanyika, UNDP imeahidi kuwapiga msasa waandishi wa habari kutoka MCL na Azam Media ili kuwaongezea ujuzi na kuwafanya kuwa wabobezi katika kuripoti habari za ubunifu.

Mkurugenzi wa Fedha kutoka Vodacom Tanzania, Hilda Bujiku amesema kupitia wiki ya ubunifu Tanzania wanalenga kuleta mabadiliko kwa kukuza ubunifu, kuwezesha jamii na kujenga ustahimilivu.